Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bajeti ujenzi barabara Ruangwa sasa Sh4.8 bilioni

Fedhapic Bajeti ujenzi barabara Ruangwa sasa Sh4.8 bilioni

Fri, 29 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imeongeza bajeti ya ujenzi wa barabara za ndani katika Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi kutoka Sh1 bilioni hadi Sh4.8 bilioni.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa Desemba 29, 2023 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Litama, Ruangwa mkoani Lindi.

“Rais Samia Suluhu Hassan ametuongezea fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara za ndani, hivyo tuna Sh4.8 bilioni,” amesema Waziri Mkuu na kuongeza;

“Niwape siri, Rais Samia ametuunganisha Masasi na Ruangwa kupitia ujenzi wa barabara ya Nanganga-Ruangwa na kilomita 38 zimejengwa, pia ametupa fedha kwa ajili ya kuunganishwa Ruangwa na Nachingwea kwa kiwango cha lami.”

Septemba 18 mwaka huu akiwa katika ziara wilayani Ruangwa, Rais Samia aliweka jiwe la msingi ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami Ruangwa – Nanganga yenye umbali wa kilomita 53.3.

Akizungumza na wakazi wa kijiji cha Juhudi B kwenye kata ya Chinongwe, Ruangwa mkoani Lindi, Majaliwa amesema Serikali imeweka msisitizo katika kuendeleza sekta ya kilimo kwenye mazao ya chakula na biashara.

Amesema lengo ni kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa chakula na kila Mtanzania anayejishughulisha na kilimo akuze kipato chake na uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Amesema Rais Samia wakati wote amedhamiria kuhakikisha Tanzania inakuwa kimbilio la wengine wanaohitaji chakula.

“Tumuunge mkono Rais wetu kwenye mapambano yake ya kukuza sekta ya kilimo, amefanya makubwa kwenye sekta ya kilimo ikiwemo kuagiza kutengwa kwa maeneo ya kilimo kwa ajili ya vijana,” amesema Majaliwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live