Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bajeti Kuu yaleta kicheko kwa Machinga, kilio mikopo ya vijana

PICHA YA MACHINGA Bajeti Kuu yaleta kicheko kwa Machinga, kilio mikopo ya vijana

Thu, 16 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hakuna tamu isiyo na chungu, ndivyo unavyoweza kusema juu ya mgawanyo mpya wa asilimia 10 za mapato ya ndani kwa kila Halmashauri uliotangazwa na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba ambao unaonekana umewabana wanawake na vijana huku kicheko kikienda kwa kundi la wamachinga.

Akiwasilisha bajeti kuu ya Serikali bungeni jana, Waziri Nchemba alipendekeza asilimia 10 ya mapato ya ndani inayotolewa na halmashauri kama mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu imegwe na kwenda kwenye ujenzi masoko ya wamachinga.

Katika mgawanyo huo, ujenzi wa miundombinu na masoko ya wamachinga utapewa asilimia tano, wakati kundi la vijana na wanawake watapewa asilimia nne kila moja huku asilimia moja ya fedha hizo itakwenda kundi la wenye ulemavu.

Awali vikundi vya wanawake na vijana walikuwa wakipatiwa asilimia nne ya asilimia hizo 10 za mapato na asilimia mbili ilikuwa ikienda kwa vikundi vya watu wenye ulemavu, huku mgawanyo huo mpya ukiwagawa baadhi ya wananchi.

Serikali kupitia bajeti hiyo ya 2022/23, imetenga Sh45 bilioni kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa miundombinu na mtaji kwa wamachinga ambapo kila mkoa, wamachinga walioko kwenye maeneo yaliyopangwa watanufaika na Sh1 bilioni.

Mmoja kati ya vijana ambao waliwahi kunufaika na fedha hizo, Athman Ally, mkazi wa kata ya Karanga mjini Moshi, alisema huo ni mpango mzuri kwa kundi la wamachinga kwa vile unakwenda kuweka mazingira ya uhakika kwao.

“Ila hili la kushusha fedha za vijana na wanawake na kuwa asilimia nne unakwenda kuwa janga kwa vile tayari kundi hilo ndilo lilikuwa limeanza kupata mwamko wa kukopa fedha hizo na ndio kundi kubwa sana pia,” alisema.

Mjasiriamali huyo alipendekeza urudishwe mgawanyo wa awali na fedha hizo kwa ajili ya kujenga miundombinu na masoko ya wamachinga zitafutiwe chanzo kingine nje ya asilimia 10 inayotengwa na Halmashauri kutoka katika vyanzo vya ndani.

Kuluthum Ramadhan, anayejishughulisha na uuzaji wa samaki kwa kuwatembezea wateja wake majumbani, alisema amefurahishwa na uamuzi wa serikali kulitambua kundi la wamachinga na kuanza kuliwekea mazingira mazuri ya biashara.

Diwani wa Kata ya Katangara Mrere wilayani Rombo, Venance Maleli alipongeza uamuzi huo wa Serikali kuamua fedha zile za asilimia 10 za mapato ya ndani, kwamba asilimia tano ziende kwa wamachinga akisema ni jambo jema na zuri.

“Hili linakwenda kulirasmisha rasmi hili kundi ambalo kiukweli ni kubwa sana na ni watu waliojiajiri wenyewe lakini hili la asilimia mbili kwa wanawake na asilimia mbili kwa vijana ni ndogo ukilinganisha na ukubwa wa makundi hayo,” alisema.

Charles Raymond, mkazi wa Pasua na mfanyabiashara ndogo ndogo alipongeza uamuzi wa Serikali kulitazama kundi la wamachinga kwa jicho la huruma kwani kujengwa kwa masoko kutaondoa kufukuzana kati yao na Serikali.

Hadija Salum, mfanyabiashara wa bidhaa za mtumba, ikiwamo viatu na nguo, alisema fedha hizo zilizoelekezwa kwa wamachinga zitasaidia kujenga miundombinu na kupatiwa mikopo kwa kuwa amesikia Serikali imetenga Sh45 bilioni.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live