Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bajeti Kuu kujadiliwa siku mbili

4741 MPANGO BUNGEDOM Bajeti Kuu kujadiliwa siku mbili

Thu, 7 May 2020 Chanzo: --

BAJETI Kuu ya Serikali sasa itajadiliwa kwa siku mbili badala ya siku sita hadi saba kama ilivyokuwa miaka mingine. Ratiba mpya ya shughuli za kikao cha 19 cha Bunge la 11 iliyotolewa jijini hapa, imeonyesha.

Awali, ratiba ilionyesha kuwa bajeti hiyo ingesomwa Mei 29, mwaka huu na kujadiliwa kwa siku sita na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli, kufunga Bunge Juni 30.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo mpya Rais atafunga Bunge Mei 29, mwaka huu.

Ratiba ilionyesha pia kuwa Bajeti Kuu itawasilishwa bungeni Jumatano Mei 20, majira ya saa 10 jioni na mjadala kufanyia Mei 21 na 22.

Vile vile, tofauti na miaka mingine tangu kuanza kwa Bunge la 19, Mei 20, wabunge wataingia mara mbili bungeni, wakati wa asubuhi saa 4:30 na saa 10:00 jioni.

Kutokana na ratiba hiyo kwa sasa kila wizara itafanya mawasilisho yake, mjadala na kupitishwa kwa siku moja na vikao vitaanza saa 8:00 mchana hadi saa 12 jioni.

Mabadiliko hayo yalianza Aprili 20, mwaka huu, lengo ni kuwezesha shughuli kumalizika mapema zaidi.

Pia, baada ya kupitishwa kwa bajeti kuu wabunge watakwenda kwenye mapumziko ya Sikukuu ya Eid, na kurudi Mei 26, kuendelea na miswada mbalimbali.

Miswada inayotarajiwa kuwasilishwa na kujadiliwa katika Bunge hilo ni wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2020, Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa mwaka 2020.

Mingine ni Muswada wa Sheria ya Afya ya Mimea wa mwaka 2020, Muswada wa Sheria ya kusimamia na kuendeleza uvuvi wa bahari kuu wa mwaka 2020 na Azimio la kuridhia mkataba wa kimataifa wa utoaji mafunzo na vyeti vya wafanyakazi meli za uvuvi wa mwaka 1995.

Baada ya shughuli hizo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), zitafuata na Waziri Mkuu atahutubia na Rais kulifunga Bunge.

Hadi sasa wizara zilizobaki ni ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Nishati, Wizara ya Ardhi, Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Fedha na Mipango.

Chanzo: --