Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Baada ya madini na dini, JPM na wakulima

47064 Pic+jpm

Mon, 18 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Bila shaka Watanzania wote wanafurahia utaratibu aliouanzisha Rais John Magufuli wa kukutana na makundi muhimu ya kijamii au kisekta na kuzungumza nayo.

Rais amekutana na wadau wa sekta ya madini na kufanya nao mazungumzo mazito Ikulu na kisha akakutana na viongozi wakuu wa taasisi za kidini na kufanya nao mazungumzo yenye tija. Mazungumzo ya makundi yote mawili yalirushwa mubashara na vyombo vya habari.

Zungumza upendacho

Jambo moja ambalo lilinivutia kwenye utaratibu wa mazungumzo hayo ni waalikwa wote kutakiwa kuzungumza mawazo yao vile watakavyo, hakuna anayezibwa mdomo!

Atakayemueleza Rais kuwa Serikali yake inafanya vizuri anaruhusiwa, atakayemueleza Rais kuwa Serikali yake inaendeshwa vibaya anaruhusiwa, atakayemueleza Rais juu ya madhaifu na uimara wa Serikali yake anaruhusiwa.

Baada ya waalikwa kuzungumza, Rais Magufuli amekuwa na kawaida ya kujibu hoja mbalimbali, kuzibeba hoja kadhaa na kufafanua mambo mengi anayodhani yanahitaji ufafanuzi.

Huwapongeza watoa hoja wote ambao huikosoa serikali yake katika mapungufu yake ya kiutendaji na huziunga mkono hoja zenye tija zinazohusu Serikali au taasisi za kiserikali kushindwa kusimamia vizuri sekta kadhaa walizopewa.

Utaratibu huu wa Rais wa Tanzania kufanya mazungumzo makubwa na ya kina na makundi ya kijamii ni wa mfano na unapaswa kuungwa mkono na kuendelezwa. Kama huko nyuma wako watu waliokuwa wanalalamikia kukosekana kwa mazungumzo baina ya Serikali na makundi muhimu ya kijamii ili yashiriki kuishauri Serikali, watu hao wanapaswa kuboresha juhudi za sasa za ufunguaji wa milango kati ya Serikali na wao.

Mkutano na wadau wa madini

Utaratibu huu wa Rais ni utaratibu binafsi na hiyari yake yeye mwenyewe, najaribu kujenga hoja ya kuonyesha umuhimu wa utaratibu huu lakini itakayoonyesha kuwa makundi mengi zaidi yanapaswa kufikiwa na kujadiliana na mkuu wa nchi, kwa sababu kabla ya mkutano wa Rais na wadau wa sekta ya madini, jamii yetu ilikuwa inapewa taarifa nyingi halisi na potofu juu ya hali ya sekta hiyo na kila aliyeweza alihukumu upande wowote kwa kadri alivyotaka.

Wadau walipokutana na Rais na kufanya mkutano wa pamoja, kwa aliyefuatilia vyombo vya habari alibaini kuwa Serikali inafanya kazi kubwa sana ya kuhuisha sekta ya madini; yako mazuri mengi sana yanaendelea; iko mikwamo na mapungufu kadhaa yanayopaswa kushughulikiwa si na Serikali tu, hata wafanyabiashara wakubwa na wadogo, wamiliki wa migodi mikubwa na wachimbaji wadogo.

Kabla ya mkutano wa namna hiyo, kila baya lililokuwa linatokea kwenye sekta ya madini lawama zilitupwa kwa Serikali. Kipindi chote cha nyuma, ufafanuzi wa Serikali nao ulikuwa ni wa upande wake, haukuwa ufafanuzi shirikishi ule wa ana kwa ana.

Wakulima

Ziko sekta mbalimbali za kijamii ambazo Rais atapaswa, ikiwa anapenda, kukutana nazo ili kukata mzizi wa fitina. Sekta hizi ni pamoja na wakulima, nitasema kwa nini. Najua zipo nyingine nyingi lakini nina hoja ya kwa nini wakulima.

Tanzania ni nchi ambayo kitakwimu asilimia 70 ya raia wake wote wanategemea kilimo kama njia ya kujiingizia kipato na kuendeleza maisha yao ya kila siku. Hii ina maana kilimo ndicho uti wa mgongo wa taifa na kikiendelea kutegemewa na kuendesha maisha ya wananchi wengi.

Sekta hii kubwa bado inakumbwa na madhila mengi yanayosababishwa na watendaji wa Serikali, Serikali yenyewe au wakulima wenyewe. Madhila haya yanatatulika na mengine yataanza kutatulika mara moja siku wakulima wakiwekwa pamoja na wizara ya kilimo, Rais mwenyewe na watendaji wengine wanaoshughulika na kilimo.

Wakulima wa Tanzania wana malalamiko mengi sana na wizara ya kilimo haijawahi kufanya kazi kubwa ya kuwainua tangu enzi za uhuru. Katika maeneo mengi wanalima kwa shida wakikopa pesa za kupata pembejeo ambazo ni ghali na mwishoni wanazalisha mazao ambayo thamani yake ni ndogo kuliko fedha walizowekeza kwenye kilimo chenyewe, hali hii inazidisha umasikini vijijini.

Siku hiyo Rais akiwaita wakulima Ikulu na waziri wake na watendaji wake wakakaa pembeni ndipo tutajua kuwa bado wizara ya kilimo haimsaidii Rais na haijafanya kazi ya kutosha ya kuwasaidia wakulima ambao wengi wao hawana elimu wala utaalamu wa kilimo, hawana wataalamu wa kuwasimamia kufanya kilimo chenye tija, hawana mitaji na pembejeo, hawana mashine za kisasa wala teknolojia za kufanya kilimo, hawana maghala, hawana masoko wala hawana nyenzo muhimu za kuwakwamua kutoka kwenye umasikini kupitia kwenye kilimo.

Natamani kuona siku moja wizara ya kilimo inalionyesha taifa hili mipango yake ya muda mrefu na muda mfupi ya kupambana na changamoto za wakulima. Haiwezekani miaka inakwenda mbele lakini changamoto za wakulima ziko pale pale na ama zinaongezeka.

Haiwezekani kuwa tunao wataalamu wa kilimo wamejaa vijijini wanalipwa mishahara na Serikali lakini hawatimizi wajibu wao inavyopaswa. Siku wakulima wakikaa na Rais na waziri na watendaji wa wizara, ndipo mkuu wa nchi atajua kuwa anayo kazi ya ziada ya kupanga na kupangua safu na mipango ya kilimo cha nchi hii.

Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Mfuatiliaji wa Utendaji wa Serikali barani Afrika; ni Mtaalamu Mshauri wa Miradi, Utawala na Sera. Ni Mtafiti, Mfasiri, na Mwanasheria. Simu; +255787536759 (Whatsup, na Meseji)/ Barua Pepe; [email protected] )



Chanzo: mwananchi.co.tz