Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

BRELA yajivunia kuondoa urasimu

BRELA TZ BRELA yajivunia kuondoa urasimu

Sun, 5 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAKALA wa Usajili wa Leseni na Biashara (BRELA), umejivunia kuondoa urasimu kwenye upatikanaji wa leseni hali ambayo imeondoa malalamiko yaliyokuwapo awali na watu sasa wamekuwa wakipata leseni kwa wakati.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa, alisema hayo jana wakati akizungumza kwenye Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara, yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Nyaisa alisema hivi sasa wameweka mazingira mazuri na hakuna mfanyakazi anayeweza kuzembea na kusababisha usumbufu kwa mteja hivyo amewakaribisha wanaotaka kusajili biashara mpya na kampuni kujitokeza kwa wingi.

“Tumeamua kuwatumikia Watanzania kwa dhati kabisa na kwetu pale tukigundua mtumishi wetu wamefanya jambo baya kwa mteja hakuna cha nini wala nini tunamuondoa kwasababu tumeamua kufanyakazi,” alisisitiza Nyaisa.

Aidha, alisema wameweka vijana mahiri ambao wamekuwa wakiingia kwenye mitandao na kuchukua hoja za wananchi mbalimbali na kuziwasilisha kwa wataalamu ambao huzijibu.

Alisema hali hiyo ndiyo imeondoa misururu ya wananchi waliokuwa wakijazana kwenye ofisi za taasisi hiyo kwaajili ya kupata majibu ya maswali mbalimbali waliyokuwa nayo wakati huo.

“Brela tunawategemea sana wateja wetu, ndiyo maana hatutaki urasimu wala rushwa kabisa watu waje hata huku sabasaba watapata majibu ya hoja zote walizonazo maana timu nzima iko huku kwaajili ya kuwasikiliza,” alisema Nyaisa

Alisema miongoni mwa maboresho waliyoyafanya ni kuhakikisha shughuli zote zinafanyika kwa njia ya mtandao ili wananchi wasipate usumbufu wa kwenda kwenye ofisi hizo kupanga foleni kwaajili ya kusubiri huduma zao.

Alisema wameweka mifumo ya utendaji kazi ambapo mtumishi wa Brela halazimiki kukutana na mteja kwani anaweza kujisajili kwa njia ya mtandao popote alipo na kupata cheti cha usajili kwa mtandao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live