Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

BRELA yaanika 'Wajanja wa mjini'

Brela Msz BRELA yaanika 'Wajanja wa mjini'

Fri, 21 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wanapiga pesa kiulaini!Hivyo ndivyo unavyoweza kuelezea kuhusu baadhi ya watu ambao wamekuwa wakiingia katika mfumo wa mtandao wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni(BRELA) na kisha kusajili majina ya kampuni na biashara.

Wajanja hao wanaojua vizuri faida za kusajili jina la biashara au kampuni wakishakamilisha sajili hizo wanasubiri kupiga pesa kiulaini kwasababu wamekuwa wajanja kwani wakati mwingine wanaangalia biashara au kampuni ambazo hazijasajiliwa na wao wanakimbilia kusajili.

Wakishafanya usajili wanasubiri wahusika ambao wamekuwa wakifanya biashara ambazo zimeshapata umaarufu lakini hawajasajli majina ya biashara au kampuni, hivyo kinachofuata ni mazungumzo na fedha lazima itaingia mifukoni mwa wajanja wanaojua umuhimu wa kusajili jina la biashara kisheria.

Hayo yamebainika Juni 19,2024 mkoani Morogoro wakati Mkuu wa Sehemu ya Kampuni kutoka Kurugenzi ya Kampuni na Majina ya Biashara wa BRELA Lameck Nyange akiwasilisha mada iliyohusu majina ya biashara na umuhimu wa kusajili.

Wakati anaeleza kuhusu usajili wa jina la biashara, Nyange amesema kuna baadhi ya watu ambao wamekuwa wakisajili majina ya biashara na kisha kusubiri kupata pesa na wanafanya hivyo baada ya kuangalia fursa katika jina la biashara ambalo anasajili.

“Kuna watu ambao wanafanyabiashara zao na zimekuwa maarufu lakini hawajasajili hivyo kuna watu wanaingia katika mfumo na kisha kusajili. Anapokuja mhusika kutaka kusajili anakuta tayari jina limesajiliwa, hivyo inabidi amtafute aliyesajili na hapo wataingia katika mazungumzo na ndipo wanapopata fedha.

“Ndio maana BRELA tumekuwa tukitoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kusajili jina la biashara kwani tunalo daftari lenye orodha ya majina yote ya biashara na kampuni ambazo zimesajiliwa.Hivyo mtu anapokuja kusajili tunaingia kwenye mfumo na kuangalia kama tayari jina hilo la biashara limesajiliwa au laa.

“Kuna faida nyingi za mfanyabiashara kusajili jina la biashara na moja ya faida kubwa ni ulinzi wa jina lake maana BRELA tunaposajili jina la biashara tunalilinda na hivyo linakuwa katika ulinzi na kwa mwaka gharama ya jina la biashara ni Sh.5000 tu.Sajilini majina yenu ya biashara kwani hata anapotaka kulitumia ni rahisi kwenda kushitaki mahakamani,amesema Nyange.

Akifafanua zaidi amesema watu wanafanyabiashara kwa kutumia majina yasiyosajiliwa na hivyo hawana ulinzi wa kulindwa.“Anayepewa ulinzi ni yule ambaye amesajili. Mtu anaweza kuja kusajili jina lake na wala halifanyii kazi na sheria haijatoa mamlaka ya kufuatilia kwanini aliyesajili jina la biashara halifanyii kazi.

“Ili kupata ulinzi wa kisheria unapaswa kuwa umesajili jina lako la biashara na mtu mwingine akalitumia unaweza kumshitaki mahakamani.Hivyo faida mojawapo ya kusajili jina la biashara ni kupata haki ya kumshitaki aliyetumia jina lako.”

Kuhusu faida za kusajili jina la biashara mbali ya kuwa umewelika katika ulinzi, pia inasaidia mhusika kupata fursa mbalimbali zikiwemo za kifedha kama kupata mkopo lakini faida nyingine mtu anakuwa amefanya biashara muda mrefu na amekuwa maarufu lakini kwasababu hujasajili mtu mwingine anasajili, hivyo ukisajili hakuna anayeweza kusajili tena.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live