Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

BOT kununua tani 6 ya dhahabu

BOT Kununua Tani 6 Ya Dhahabu BOT kununua tani 6 ya dhahabu

Fri, 22 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Benki Kuu ya Tanzania imeanza zoezi la ununuzi wa dhahabu kwa lengo la kuchangia maendeleo ya sekta ya madini nchini pamoja na kuongeza akiba ya fedha za kigeni.

Akizungumza baada ya ziara katika kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Geita (Geita Gold Refinery) na kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Mwanza (Mwanza Precious Metals Refinery Co. Ltd), Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, amesema kuwa tayari BoT imenunua na kusafisha dhahabu yenye uzito wa kilo 418.

“Kama alivyoeleza Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba kwenye bajeti, serikali imetenga fedha kwa ajili ya kununua dhahabu na mwaka huu tumepanga kununua tani sita ya dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo, wakati na wakubwa , alisema.

Gavana Tutuba aliongeza kuwa kupitia Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa Ajili ya Mauzo ya Bidhaa za Nje ya Nchi (Export Credit Guarantee Scheme), BoT imetenga pesa kwa ajili ya kuongeza mauzo nje pamoja na kuboresha bidhaa zinazoagizwa nje ya nchi ziweze kuzalishwa na kuuzwa ndani ya nchi.

“Tumefanya majadiliano ili tuangalie namna tunavyoweza kuwasaidia wachimbaji wadogo ili wapate fedha, wachimbe na kuuza kwenye viwanda vya kusafisha dhahabu ili itakapo chujwa iweze kuuzwa kwa Benki Kuu,” alisema.

Vilevile, Gavana Tutuba amewaasa wauzaji wakubwa wa dhahabu kuzingatia sheria ya fedha za kigeni ambayo i inawataka kuleta nchini fedha za kigeni zinazopatikana katika mauzo ya dhahabu ndani ya siku 90 ili ziweze kusaidia ukuaji wa uchumi wetu.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dkt. Venance Mwasse, ameishukuru Serikali kwa kuwezesha ujenzi wa viwanda vya kusafisha dhahabu nchini ambapo kupitia viwanda hivyo, Benki Kuu ya Tanzania itaweza kununua na kuhifadhi dhahabu na kuongeza akiba ya fedha za kigeni ili kuimairisha uchumi wa taifa kwa ujumla.

“STAMICO tutashirikiana na Benki Kuu kuhakikisha kwamba wachimbaji wadogo wanapata udhamini wa mikopo kwa ajili ya kuwawezesha kuchimba dhahabu zaidi na kuileta katika kiwanda chetu cha kusafisha dhahabu cha Mwanza ili Benki Kuu ipate dhahabu zaidi kwa ajili ya kutunza kwenye hifadhi yetu, alisema.

Benki Kuu ya Tanzania inashiriki katika Maonesho ya Sita ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika Viwanja vya Bombambili vilivyopo Mkoani Geita kuanzia tarehe 20 hadi 30 Septemba, 2023. Maonesho haya ni fursa adhimu ya kuimarisha ushirikiano kati ya Benki Kuu na sekta ya madini nchini.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live