Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

BARAZA LA SALIM: Watanzania hawataki maneno, muhimu ni vitendo

54906 Pic+maneno

Wed, 1 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Baada ya muda fulani hutokea taarifa ambazo ninapozitafakari hupata taabu kujua mantiki yake.

Wakati mwingine hujikuta ninajiuliza kama ilikuwapo haja ya kufanya hivyo au waliofanya hivyo walifanya uchambuzi kwa kiasi gani kufikia uamuzi huo?

Miongoni mwa maamuzi ya karibuni yaliyonipa taabu kufahamu mantiki yake ni uamuzi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Zanzibar

kuunda kamati inayoratibu sukari inayozalishwa katika kiwanda cha Mahonda kiliopo Kaskazini Unguja.

Sukari hiyo imekuwa mada ya kulaumiana kati ya pande hizi za Muungano baada ya kupigwa marufuku kuingia Bara.

Hapo awali tuliambiwa uamuzi huo ulifanyika kwa ‘’nia njema’’ ya kuisaidia Zanzibar isipate shida ya sukari kwa vile hiyo inayozalishwa na kiwanda hicho haitoshelezi mahitaji ya watu wa Visiwani.

Sasa tumeambiwa na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud, kwamba lengo ni kujua ubora wake na kuhakikisha kwamba kiwanda hicho hakiagizi sukari kutoka nje na kuisafirisha Bara ili kufanya biashara.

Sijui niamini maelezo yepi, yale yaliotolewa hapo kwanza au hili ninalolisikia hivi sasa na kupelekea kuundwa kamati maalumu ya sukari.

Ninachokiona ni kuendeleza utamaduni uliozoeleka nchini kwa kila jambo lenye utata kuundiwa kamati ndogo, tume ya uchunguzi au ya maelewano.

Lakini hatimaye tunaona mapendekezo yanayotolewa na hivyo vikundi kuwekwa kapuni kama vile palikuwa hapana haja ya kuundwa vyombo hivi.

Waziri amesema kamati itachukua hatua za kuondoa vizingiti vinavyokwamisha sukari inayozalishwa Mahonda ambayo inasemekana kupendwa sana Bara kwa uzuri wake kuingia soko la upande huo wa pili wa Muungano.

Sidhani huu mtindo wa kuunda kamati kushughulikia bidhaa moja ni sahihi na umeanzisha utaratibu wenye manufaa.

Hii ni kwa sababu hata maji yanayozalishwa katika viwanda vya Zanzibar nayo yamekumbwa na vizingiti hivi. Je, nayo yataundiwa kamati maalum?

Wasiwasi wangu ni kwamba tunaweza kujikuta kila bidhaa moja inapozuiwa kusafirishwa kutoka sehemu moja ya Muungano kwenda nyingine tunaunda kamati.

Hatmaye tunaweza kuwa na kamati maalumu za chumvi, viazi, mananasi, karafuu, mafenesi na bidhaa nyengine.

Ni vizuri pakatengenezwa mfumo wa biashara utakaokuwa wazi na kuepukana na leo bidhaa hii kuziliwa Bara au ile kuingia Visiwani.

Mwananchi wa kawaida haelewi kwa nini katika leo katika eneo tunaloliita nchi moja baada ya sehemu hizi mbili za Tanzania kuungana pawepo na vikwazo vya biashara wakati hakuna vizingiti vya aina hiyo

kwa bidhaa zinazotoka nchi za jirani na kwingineko.

Hili suala la sukari ambalo sasa limeundiwa kamati ambayo itakuwa na vikao vya mara kwa mara na kutumia fedha za walipa kodi ni miongoni mwa yale mambo yanayoorodheshwa kuwa ni kero za Muungano.

Kwa bahati mbaya kila siku tunasikia serikali zetu mbili kuwepo mbioni kumaliza tatizo, lakini tunaomba mambo yapo vilevile licha ya kuahidiwa pamepatikana suluhisho.

Watanzania wa pande zote mbili wamechoshwa na mivutano na wanataka uwepo mfumo ambao utapelekea hizo zinazoitwa kero za Muungano tulizoanza kuzisikia miaka 55 iliyopita zinamalizika.

Kama ni kuundwa tume, kamati kubwa na ndogo hili imefanyika sana na mara nyingi hatuoni mapendekezo yanayolewa kufanyiwa kazi.

Kinachosikitisha ni kuona yanatiwa kapuni na wakati mwingine wajumbe waliotoa mapendekezo husakamwa na kutolewa kauli zisizopendeza.

Watu hawa hulaumiwa kama vile wamejipa kazi hiyo wenyewe na si kutumwa na serikali zetu kuifanya kazi hiyo.

Wakati umefika tujitahidi kuondosha moja kwa moja hizi zinazoitwa kero za Muungano ili Watanzania wawe na imani kwamba umoja wetu hauna mushkeli na ni watu wanaoishi pamoja na kushirikiana kwa raha na furaha.

Watanzania hawataki kuona kila siku tunaunda tume na kamati za kushughulikia kero za Muungano. Wanachotaka ni kwa hizo zinazoitwa kero zinakuwa sehemu ya historia ya nchi yetu.



Chanzo: mwananchi.co.tz