Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Azania waomba wana saikolojia

17e82bdc07fd061f10f2fa6846e77aa2 Azania waomba wana saikolojia

Mon, 14 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KUTOKANA na wimbi la vijana kujiua, wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Azania jijini Dar es Salaam wameomba wahitimu wa shule hiyo wa mwaka 1992 kuwapatia wataalamu wa kutoa nasaha na saikolojia.

Ombi hilo lilitolewa na Rais wa wanafunzi wa shule hiyo, Salum Sharif wakati wahitimu hao wa mwaka 1992 walipokabidhi kompyuta 10 kwa shule hiyo, ikiwa ni muendelezo wa utaratibu waliojiwekea wa kuisaidia shule hiyo waliosoma zamani kila mwaka.

“Tunashukuru kaka zetu na baba zetu kwa kutujali na kutupatia kompyuta, lakini nina ombi moja, tunaomba mtusaidie mtu wa kutupatia nasaha na saikolojia ya maisha, sisi kama vijana tuna changamoto nyingi zinazotukabili na inafikia baadhi yetu kukatisha hata maisha, ila tukipata watu wa nasaha hata mara moja au mbili kwa mwaka wakazungumza na sisi itasaidia,” alisema.

Kwa mujibu wa tafiti za Shirika la Afya Duniani (WHO), kila sekunde 40 mtu mmoja hupoteza maisha kwa kujiua.

Kiwango cha wastani cha kujiua duniani kwa mwaka 2016 kilikuwa ni watu 10.5 kwa kila watu 100,000. Hata hivyo viwango vilikuwa na tofauti kubwa, kati ya nchi na nchi kutoka kwa watu watano wanaojiua kati ya watu 100,000 hadi kufikia zaidi ya watu 30 kwa watu 100,000.

Wakati asilimia 79 ya visa vya kujiua kote duniani vilitokea katika nchi za kipato cha chini na cha kati, huku nchi za kipato cha juu zilikuwa na viwango vya juu kwa watu 11.5 kati ya watu 100,000.

Awali, wakikabidhi vifaa hivyo Mwenyekiti mstaafu wa Azania Alumni 92, Daud Mayocha alisema kompyuta walizokabidhi zina thamani ya Sh milioni 14 zilizotokana kuchangishana katika kundi lao la WhatsApp.

Alisema huo ni utaratibu wao wa kawaida, ambapo huu ni mwaka wa tatu. Mwaka juzi walitoa vitabu 300, mwaka jana walitoa madawati 100 na mwaka huu wamekabidhi komyuta hizo 10.

“Sisi tumeamua kuisaidia shule yetu na wadogo zetu, tunajinyima, tunakabana mashati kidogo kinachopatikana tunarudisha kwa shule yetu, hivyo tunaomba watoto wetu na wadogo zetu msome, tunataka Azania irudi kwenye viwango vyake, 10 isikosekane kila mwaka.” alisema

Chanzo: habarileo.co.tz