Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Azam, Serikali wafikia muafaka kodi ya maziwa

44340 Pic+maziwa.png Azam, Serikali wafikia muafaka kodi ya maziwa

Fri, 1 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baada ya kuacha kuagiza kwa miezi sita na kusababisha kutoweka sokoni, maziwa ya Azam yataanza kupatikana kuanzia leo baada ya Serikali kuipa unafuu wa tozo ya kuingiza bidhaa zake Tanzania Bara.

Nafuu hiyo ya asilimia 87.5 imetolewa kwa ajili ya kuishawishi kufanya biashara na kujenga kiwanda Bara, ikiwa ni kati ya makubaliano.

Azam Dairies ilisitisha kuingiza maziwa yake inayoyazalisha visiwani Zanzibar Agosti mwaka jana kutokana na kushindwa tozo ya Sh2,000 kwa kila lita kwa mujibu wa kanuni za Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Lakini meneja mkuu wa Azam Dairy, Adilson Fagundes amesema baada ya mazungumzo yaliyofanyika baina ya kampuni hiyo na Serikali, muafaka umepatikana na sasa wateja wao wa Bara wataendelea kuyapata kama ilivyokuwa awali.

“Kwa makubaliano tuliyofanya, mzigo utaanza kuingia Bara Machi Mosi (leo). Kutokana na mabadiliko ya tozo za kuyaingiza huku, tulilazimika kuyauza Zanzibar tu,” alisema Fagundes.

Kwa makubaliano yaliyofanywa, kampuni hiyo imepewa punguzo la asilimia 87.5 hivyo italipa Sh250 kwa lita moja badala ya Sh2,000 iliyopo kwa mujibu wa kanuni za wizara.

Unafuu huo umetolewa pamoja na masharti kadhaa ambayo Azam itapaswa kuyatekeleza.

Na ingawa inao mkakati wa kuwa na tawi la uzalishaji kati ya mikoa ya Dar es Salaam au Pwani, mkataba uliosaniwa kati yake na Serikali unaitaka Azam Dairies kununua maziwa kutoka Kampuni ya Ranchi ya Taifa (Narco).

Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), Dk Sophia Mlote alisema unafuu huo umetolewa kwa kampuni ya Azam pekee ukiwa ni mkakati wa kuishawishi kuendelea kufanya biashara na kujenga kiwanda cha maziwa Bara.

“Tunahitaji waendelee kufanya biashara kwa faida ya Taifa ikiwamo kuongeza ajira na soko la maziwa ya wafugaji,” alisema Dk Sophia.

Katika makubaliano yaliyofanyika kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Azam Februari 22, Dk Sophia alisema Azam watalazimika kununua maziwa kutoka Narco kisha kuyapeleka Zanzibar kwa ajili ya usindikaji.

Takwimu za wizara zinaonyesha Tanzania inazalisha lita bilioni 2.4 za maziwa kwa mwaka, ingawa mahitaji yake ni takriban lita bilioni 11. Hata hivyo, viwanda vilivyopo vinasindika lita 150,000 ingawa uwezo wake ni lita 750,000 kwa siku.

Kiwanda cha Azam chenye uwezo wa kusindika lita 180,000 kwa siku, kutokana na upatikanaji wa malighafi, huchakata kati ya lita 20,000 na 25,000.



Chanzo: mwananchi.co.tz