Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Azalisha funza, awatumia kunenepesha kuku

9d39d4647bd6220cdc425c52acc005ed Azalisha funza, awatumia kunenepesha kuku

Sun, 16 Jan 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kijana Rodney Mwasha mkazi wa Mkoani wilayani Kibaha, mkoani Pwani amegundua lishe kwa kuku kwa kutumia funza anaowazalisha na kuwanenepesha kuku wa kienyeji anaofuga na kuwauza.

Akizungumza na gazeti hili mjini Kibaha alisema kuwa kutokana na kutumia funza, anapunguza gharama ya kununua lishe ya kuku kwani wadudu hao ni lishe tosha.

Mwasha alisema kuwa funza wamesaidia kuku kunenepa na amekuwa akiwauza kwa Sh 20,000 aliyotaja kuwa ni bei nzuri kwa kuku mmoja.

“Nilifikia hatua ya kuwalisha kuku funza baada ya kuona kuku kila ninapowaachia hutafuta uchafu na kula hao wadudu ndipo nilipogundua na kuanza kuwazalisha kisha kuwapa kuku wangu,” alisema Mwasha.

Alisema kuwa gharama ya kuwanunulia vitamini sasa haipo na kwa mwezi alikuwa akitumia gharama kubwa kununua lishe ili kuboresha afya ya kuku.

“Baada ya kufanya utafiti na kugundua kuwa funza ni lishe nzuri nilianza kuwazalisha funza kwa wingi na kuwapa kuku na wanakuwa na afya nzuri na wananenepa,” alisema.

Aidha, alisema kuwa funza hao anawazalisha kupitia mabaki ya vyakula, matunda na uchafu wa aina mbalimbali.

“Tangu nianze kuwalisha kuku wangu funza nimekuwa na wateja wengi kwani wamekuwa na afya na ni wakubwa wana nyama za kutosha,” alisema.

Aliongeza kuwa pia anatumia magamba ya konokono na kuyasaga kisha kuchanganya na pumba na kuwalisha kuku wake.

“Magamba ya konokono yakisagwa na kuchanganywa na pumba ni chakula kizuri sana kwa mifugo wakiwemo kuku ambapo mimi huwa nawalisha kuku wangu,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live