Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aweso aapa kutowavumilia makandarasi wazembe kumtilia ‘kitumbua mchanga’

10571 Pic+aweso TanzaniaWeb

Tue, 7 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso amesema hayupo tayari kutumbuliwa na Rais John Magufuli kwa sababu ya uzembe wa makandarasi wanaochelewa kukamilisha miradi ya maji.

Akizungumza juzi wakati akikagua mradi mkubwa wa maji kutoka Mto Ruvu hadi Orkesumet makao makuu ya wilaya ya Simanjiro, Aweso aliwataka makandarasi kufanya kazi kwa ubora.

Mradi huo unaotekelezwa na kampuni ya Shoura Ltd na Interconsult na kujengwa na mkandarasi wa Jandu Plumbers ya jijini Arusha.

Aweso alisema lazima makandarasi waliopewa miradi ya maji nchini kuhakikisha wanatimiza muda waliopangiwa na wananchi wapate maji.

Alisema Serikali imetoa Dola 2.42 milioni za Marekani huku Benki ya Maendeleo ya Watu wa Uarabuni ikitoka Dola 16 milioni kwa ajili ya kuhakikisha maji yanapatikana kutoka Mto Ruvu hadi Orkesumet.

Aliwataka wasimamizi wa mradi huo ambao ni Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Babati (Bawasa) chini ya mkurugenzi, Idd Msuya kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kupunguza kero ya ukosefu wa maji safi.

“Sitakubali kutumbuliwa kwa sababu ya uzembe wa makandarasi haiwezekani tuanzishe kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani halafu nyie makandarasi mnachelewesha miradi hii, hakikisheni wananchi wanapata maji kwa wakati,” alisema Aweso.

Naye Msuya alisema mradi huo mkubwa wa maji una uwezo wa kutoa maji lita za ujazo milioni 1.5 kwa siku na kuhudumia zaidi ya wakazi 27,762 wa mji wa Orkesumet na vijiji vilivyopo jirani.

Msuya alisema Simanjiro ipo katika ukanda wa nyanda kame na kusababisha vyanzo vingi vya maji kukauka wakati wa kiangazi na vingine vikipoteza uwezo wa uzalishaji.

Awali, mkandarasi kutoka kampuni ya Jandu Plumbers, Kotturu Ramnadh alisema mradi huo ni mkubwa katika wilaya hiyo lakini wanakabiliwa na changamoto ya namna ya kupandisha maji kutoka eneo la tambarare hadi kwenye miinuko, huku akiahidi kutekeleza mkataba kulingana na wakati.

Chanzo: mwananchi.co.tz