Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Atoa siku 100 kiwanda cha ngozi kikamilika

Ngoziiiii.jpeg Atoa siku 100 kiwanda cha ngozi kikamilika

Fri, 23 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Cyprian Luhemeja ametoa siku 100 kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Wafanyakazi wa Umma (PSSSF) kuhakikisha awamu ya pili ya ujenzi wa kiwanda cha kuchakata bidhaa za ngozi kilichoko Kilimanjaro unakamilika na kuanza kufanya kazi ifikapo Julai 2024.

Ametoa agizo hilo leo Februari 22, 2024 alipokagua maendeleo ya ujenzi wa kiwanda hicho cha Kilimanjaro International Leather Industries Ltd (KLICL), ikiwa ni sehemu ya kukagua maendeleo ya miradi inayotekelezwa na serikali kupitia ofisi hiyo.

Luhemeja amesema kukamilika kwa kiwanda hicho kutaongeza thamani ya zao la ngozi ghafi, kufungua fursa za soko la ngozi kutoka kwa wafugaji na kuongeza ajira kwa vijana pamoja na mapato ya fedha za ndani na za kigeni.

Hata hivyo, ameeleza kuridhishwa na ubora wa bidhaa zinazozalishwa kiwandani hapo na kutoa wito kwa Watanzania kuwa na utamaduni wa kuthamini bidhaa zinazozalishwa nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Abdul-Razaq Badru ameahidi kutekeleza maagizo hayo akisema PSSSF kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza watahakikisha wanakamilisha awamu ya pili ya ujenzi wa kiwanda hicho ili Watanzania wanufaike nacho.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live