Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Athari za corona kwa mazao yanayosafirishwa nje zatajwa

CORONA Athari za corona kwa mazao yanayosafirishwa nje zatajwa

Wed, 6 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WIZARA ya Viwanda na Biashara, imeeleza athari za kiuchumi zilizosababishwa na janga la corona katika mazao ya biashara yanayosafirishwa kwenda nje.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2020/21, Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, alisema biashara hizo hutegemea usafiri wa anga kuingia katika nchi mbalimbali ambao kwa sasa haupo, ikiwa ni jitihada za kujikinga na corona.

Alisema athari kubwa zaidi ni kwenye mazao kwa kuwa Tanzania soko lake liko katika nchi za kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Ulaya (EU), Asia, China, India na Japan na AGOA, na kwamba bidhaa zinazouzwa kwa wingi ni almasi, dhahabu, chai, kahawa, maua na viungo.

Bashungwa alisema baadhi ya mazao ya kimkakati yakiwamo pamba, korosho na kokoa bei zake zimeshuka.

“Katika kipindi cha Februari na Machi 2020, bei ya pamba duniani imeshuka kwa asilimia 12, kakao kwa asilimia 22 na kahawa kwa asilimia 5 (Arabika) na asilimia 3.5 (Robusta) kutokana na kufungwa kwa maduka nchini China, Ulaya na Marekani kutokana na zuio la kutotoka nje,” alisema.

Alitolea mfano Kampuni ya Starbucks kufunga maduka 2,150 kati ya 4,300 nchini China, na kwamba mauzo ya mazao na bidhaa za kilimo yameshuka.

Aidha, alisema kiwango cha ununuzi wa kakao kilishuka kutoka tani 116,440 Februari 2020 hadi kufikia tani 38,354 mwezi Machi 2020 ikiwa ni sawa na asilimia 67.1.

Kwa upande wa wazalishaji wa mazao ya mboga, matunda, maua na viungo kwa miaka mingi wanategemea soko la nje hasa Ulaya, Marekani na Asia.

“Kutokana na mlipuko wa ugojwa huo na kufungwa kwa mipaka, kumeathiri biashara hiyo ambayo mazao yake yanaharibika kwa wepesi,” alisema Waziri Bashungwa.

Alifafanua jinsi biashara ya mazao hayo iliyoathirika kuwa ni mauzo ya mazao ya mboga na matunda nchini kumeshuka kwa asilimia 50.

“Hali hiyo imesababishwa na kushuka kwa mahitaji ya bidhaa hizo hususan katika soko la nje, na kupungua kwa safari za ndege. Mfano, Shirika la KLM limepunguza safari zake kutoka safari saba kwa wiki hadi tatu,” alisema na kuongeza:

“Uhitaji wa mazao hayo katika masoko ya ndani ni mdogo na kukosa masoko mbadala wa kupeleka bidhaa zao zaidi ya kuendelea kuzihifadhi kwa muda mfupi na baadaye kuziteketeza kabisa.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live