Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askari asimulia alivyojitosa kuzima moto hifadhi ya mafuta Lake Oil Tanzania

91273 Moto+pic Askari asimulia alivyojitosa kuzima moto hifadhi ya mafuta Lake Oil Tanzania

Fri, 10 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam.  Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini Tanzania, Wilson Mwageni ameonyesha ushujaa baada ya kufanya kitendo cha kijasiri cha kuingia kwenye eneo la matanki ya mafuta yanayowaka moto na kufanikiwa kufunga pampu ya mafuta.

Hatua hiyo ya Mwageni ilisababisha moto uliokuwa ukiwaka kwa kasi usiendelee kusambaa kwenye matanki mengine kwenye hifadhi ya mafuta inayomilikiwa na kampuni ya Lake Oil eneo la Vijibweni Wilaya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Ajali hiyo ya moto ilitokea jana usiku Jumatano Januari 8, 2020, ambapo chanzo cha moto huo na tathmini ya madhara yaliyotokea bado haijajulikana, jeshi la zimamoto na ukoaji limesema litatoa taarifa hiyo leo Alhamisi Januari 9, 2020.

Askari huyo wa kikosi cha zimamoto eneo la Kigamboni amesema baada ya kutokea moto huo na juhudi za kuzima moto zikiendelea, alipewa taarifa kuwa kuna pampu ya mafuta ambayo bado inaendelea kusukuma mafuta hayo na ili kufanikisha kupunguza madhara inatakiwa ifungwe.

Akisimulia mkasa huo, Mwageni amesema aliambia njia ya kuingilia humo ipo kwa upande wa nyuma ambapo moto huo ulikuwa bado haujawa ndipo alipoamua kumshirikisha kiongozi wake na kumwambia yeye ameamua kujitolea kwa ajili ya nchi yake na ikiwa atapoteza maisha basi watamuombea kwa Mungu.

Amesema alikuwa ameambatana na askari wenzake watatu ambao wao walihofia kuingia humo, lakini yeye aliamua kujitolea bila kujali kama angepoteza maisha ama angenusurika.

Askari huyo amesema wakati ameanza kuingia kwenda kwenye pampu hiyo ya mafuta ili akaifunge, kutokana na joto kali na moshi uliokuwa umejaa kwenye moto huo, aliwaambia wenzake wawe wanamwagia maji ili kumsaidia kupooza joto na kisha akaingia kupitia njia ya nyuma ya matanki hayo hadi akaifikia na kuifunga pampu.

Baada ya kufunga pampu hiyo na kutoka, Mwageni ameeleza kuwa kutokana na moshi kuwa mwingi eneo hilo, hali yake ilibadilika na presha ikapanda hadi akazimia kwa muda lakini wenzake walifanikiwa kumpatia huduma ya kwanza na kumhudumia hadi hali yake ya kiafya ikakaa sawa ndipo akaruhusiwa kurudi nyumbani kwake.

Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Sahar Msafiri amesema kitendo kilichofanywa na askari huyo ni cha kizalendo kwani ameokoa uchumi wa Taifa na nchi zaidi ya sita inayotumia mafuta haya.

Amesema uzalendo huo ni mkubwa na moto umedhibitiwa vizuri, “tunashukuru sana kamanda wa zimamoto kwa uzalendo wake mkubwa kwa Taifa lake.”

 

Chanzo: mwananchi.co.tz