Imeelezwa kuwa kukosekana kwa elimu ya masuala ya hisa na mitaji kwa Watanzania ni changamoto inayosababisha asilimia kubwa kuwekezaji kwenye sekta ya kilimo cha asili na mifugo.
Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Mbeya, Donald Bombo amesema hayo Juni 27, 2023 kwenye kikao cha kilicholenga kutoa elimu wawekezaji wadogo na kati iliyotolewa na Mamlaka ya Masoko, Mitaji na Dhamana (CMSA) na kufanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.
“Kukosekana kwa elimu hiyo kunasababisha asilimia zaidi ya 90 ya Watanzania kutojua umuhimu wa kuwekeza kwenye masoko ya mitaji na hisa, huku asilimia 80 wakielekeza nguvu kwenye biashara na asilimia 20 kwenye kilimo na ufugaji wa asili,” amesema.
Amesema kuna kila sababu sasa kugeukia kutoa elimu ya uwekezaji kwenye masoko ya mitaji na hisa ili jamii kuondokana na mtazamo wa kuwekeza kwenye kilimo na ufugaji wa asili ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
“Tunaona wastani wa asilimia 80 imewekezwa kwenye biashara, huku 20 kwenye kilimo na ufugaji wa asili hali hiyo ni changamoto ya Watanzania wengi kutojua umuhimu katika sekta ya uwekezaji wa mitaji na hisa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Sera, Utafiti na Mipango kutoka Mamlaka ya Masoko Mitaji na Dhamana (CMSA) Alfred Mkombo, amesema uwekezaji katika masoko ya hisa unakwenda vizuri na wananchi wanaendelea kupata uelewa mzuri ili kuona namna bora ya kubadilika.
“Changamoto kubwa ni wananchi kuelewa masoko ya mitaji na namna ya kuyatumia kwa wawekezaji hususan hati fungani na ndio sababu ya kuwakutanisha kuwapatia elimu,”amesema.
Amesema tayari wameifikia mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Zanzibar na sasa Mbeya huku matarajio yao ni kuona Mkoa wa Mbeya ukifanya vizuri zaidi katika masuala ya mitaji, hisa na kutumia fursa hiyo kuonganishwa na mifumo rasmi,”amesema.
Mfanyabishara Rose Mulyahela amesema changamoto kubwa wananchi wanatamani kuwekeza lakini shida ni mitaji na wameomba kupitia mafunzo hayo ikawe mwarobaini wa kufikia malengo.
“Serikali kupitia elimu tunayopewa iangalie namna bora ya kusaidia wawekezaji wadogo wa makampuni wanatoka sehemu moja kwenda nyingine ili kufikia malengo ya kuwekeza katika masoko ya hisa na mitaji,” amesema.