Imeelezwa kuwa asilimia 40 ya Watanzania waishio vijijini hawajafikiwa na elimu ya huduma za kifedha hali inayochangia kwa kiasi kikubwa watu wengi kushindwa kuzifikia fursa zilizopo katika sekta hiyo nchini.
Hayo yamesemwa leo Novemba 15,2022 jijini Dodoma na Kamishna wa Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Charles Mwamwaja wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa inatarajiwa kuanzia Novemba 21 hadi 26 katika viwanja vya Rock City Jijini Mwanza.
Dk. Mwamwaja amesema kutokana na hali hiyo serikali iliaandaa mpango wa miaka mitano wenye lengo la kufanya maadhimisho kila mwaka kwa lengo la kutoa elimu ya huduma za kifedha kwa umma.
”Katika asilimia hiyo ya wananchi ambao hawajafikiwa na elimu ya fedha serikali iliandaa mpango huo mwaka 2021 kwa kuandaa maadhimisho ambayo yanawakutanisha watoa huduma za kifedha nchini.”amesema Dk. Mwamwaja
Aidha ametaja malengo ya wiki hiyo ya huduma za fedha kuwa ni kujenga uelewa na weledi kwa umma katika matumizi sahihi ya huduma za fedha zinazotolewa ili kujenga uchumi na kuondoa umaskini.
”Tunalenga kuimarisha ufanisi wa masoko ,kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha, kuwezesha wananchi kusimamia vizuri rasilimali fedha na kuwezesha wajasiliamali wadogo kuongeza ujuzi na matumizi sahihi ya huduma za kifedha katika kukuza biashara zao.”amesema.
Hata hivyo ametaja washiriki wa maadhimisho hayo kuwa ni wadau wa sekta ya fedha, taasisi za fedha, Asasi zisizo za kiserikali, Saccos, wajasiliamali, vikoba, mifuko ya hifadhi ya jamii na watoa huduma za kifedha kwa njia ya mtandao.
Aidha Dk. Mwamwaja,ametoa kwa wananchi wote hususani wale wanaoishi Kanda ya Ziwa kushiriki maonesho hayo kikamilifu ili kuweza kupata elimu hiyo muhimu katika kukuza uchumi wao na wa Taifa kwa ujumla.