Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) ameipongeza Kampuni ya Sukari Kilombero ambayo inazalisha asilimia 26 ya sukari inayotumiwa hapa nchini, na kuwataka kuweka mazingira mazuri kwa wakulima ili uzalishaji huo uongezeke.
Waziri Kijaji ametoa pongezi hizo Agosti 10 mwaka huu alipotembelea kiwanda hicho akiambatana na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Kighoma Malima pamoja na Uongozi wa Wilaya ya Kilombero.
Ziara hii ni ya kwanza kwa Waziri Kijaji kiwandani ambapo ameweza kujionea uzalishaji wa Sukari na Ethanol katika viwanda vilivyopo ndani ya eneo la kampuni sambamba na maendeleo ya mradi wa upanuzi ambao kwa sasa umefikia asilimia 60.
Waziri huyo amesema nchi ina viwanda vikubwa zaidi ya vitano ambavyo vinazalisha sukari lakini asilimia 26 ya sukari inazalishwa na Kiwanda cha Sukari Kilombero.
Kijaji ameipongeza Kampuni kwa kazi nzuri na kwa uwekezaji mkubwa katika upanuzi wa kiwanda ambao utaifanya kampuni kuwa mzalishaji mkubwa wa sukari Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.
“…niwapongeze uongozi na wawekezaji wa Kampuni ya Sukari Kilombero kwa kazi nzuri inayoendelea kufanyika…wao ni wazalishaji wa asilimia 26 ya sukari yote tunayotumia ndani ya nchi yetu…” amesema Waziri Kijaji.
Aidha, Waziri huyo amepongeza kazi kubwa ya ujenzi wa kiwanda kipya ambacho kitakuza zaidi uzalishaji wa sukari katika Kampuni hiyo kutoka tani 126,000 za sasa hadi kufikia tani 271,000 kwa mwaka.
Ujenzi wa kiwanda hicho unaogharimu takriban TZS. Bilioni 566 utatoa soko la uhakika kwa wakulima wa miwa katika maeneo hayo. Kwa sasa kampuni inachakata tani takriban 600,000 za miwa kutoka kwa wakulima wa Kilombero ambapo inahitajika nyongeza ya tani 900,000 ili kukidhi mahitaji baada ya kukamilika kwa kiwanda kipya.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amepongeza mikakati iliyowekwa na uongozi wa kiwanda hicho kwa kuwapatia elimu wakulima kupitia maafisa ugani ambao wanachochea uzalishaji wa miwa wenye tija.