Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ashauri ngano kuwa zao la kimkakati

D1638f4972f4f331b0cb3604a56934c7 Ashauri ngano kuwa zao la kimkakati

Fri, 20 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SERIKALI imetakiwa kulifanya zao la ngano kuwa la kimkakati na kutumia mbegu za hapa nchini zilizo na uwezo wa kuzaa vizuri kati ya magunia 15 hadi 18 kwa ekari moja ili kuokoa fedha nyingi zinazotumika kuagiza bidhaa hiyo nje ya nchi.

Ushauri huo ulitolewa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Kituo cha Uyole kilichopo Mbeya, Dk Tulole Bucheyeki alipokuwa akizungumza na HabariLEO mjini hapa jana.

Alisema serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kuagiza ngano nje ya nchi wakati kupitia kituo hicho cha utafiti inaweza kuwafanya wakulima wazalishe zaidi hivyo kuipunguzia gharama ya kuagiza bidhaa hiyo nje ya nchi na kuokoa fedha nyingi za kigeni.

Alisema uzalishaji wa ngano wa ndani unakidhi mahitaji kwa asilimia 10 tu hivyo serikali kulazimika kuagiza asilimia 90 iliyobaki kutoka nje ya nchi.

Mtafiti wa zao la ngano katika kituo hicho, Hosea Nyato alisema ili kupata mavuno mengi, mkulima anapaswa kuzingatia kanuni za kilimo bora cha zao hilo ikiwamo kuandaa shamba muda mwafaka, kuandaa mbegu bora zinazofaa kwa eneo na mazingira ya mahali husika.

“Pia wakulima wanapaswa kutumia mbolea kiwango cha kutosha na aina sahihi za mbolea za kupandia na kukuzia,” alisema.

Lusungu Paulo kutoka Idara ya Uenezaji wa Teknolojia na Mahusiano wa kituo hicho, alisema wanaendelea kusambaza teknolojia mbalimbali za zao la ngano kwa wakulima kupitia Kituo cha Utafiti Uyole, Maonesho ya Nanenane, Maonesho ya Kilimo Biashara na katika vituo vidogo vya utafiti vilivyo chini ya taasisi hiyo.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dk Geofrey Mkamilo alisema taasisi hiyo inahakikisha teknolojia mbalimbali ambazo zimegunduliwa zinawafikia wakulima na wadau wengine katika mnyororo wa thamani.

Alisema ili kilimo kiweze kuchangia uchumi wa kaya na taifa kwa ujumla, mkulima anatakiwa aachane na kilimo cha kujikimu na kulima cha kibiashara.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TARI, Dk Yohana Budeba alisema kilimo ni uti wa mgongo nchini, hivyo anaipongeza serikali kwa kuanzisha taasisi hiyo kwani imeleta mageuzi ya kilimo na kujibu changamoto za wakulima kupitia tafiti zinazofanywa.

Chanzo: habarileo.co.tz