Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Asali ya Tanzania yapata soko SADC

70591 Asali+pic

Fri, 9 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Asali ya Tanzania inayozalishwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), imepata soko katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya kusini mwa Afrika(SADC), kupitia maonyesho ya bidhaa katika siku ya mwisho ya wiki ya viwanda kwa nchi 16 za jumuiya hiyo Jijini Dar es Salaam.

Mbali na nchi za SADC, pia wafanyabiashara kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki waliotembelea banda hilo wameonyesha nia ya kununua bidhaa hiyo.

Akizungumza na Mwananchi jana Alhamisi Agosti 8, 2019 katika banda la TFS lililopo Kituo cha Kimataifa cha Julius Nyerere(JNICC), Meneja Masoko na Uwekezaji wa wakala huo Mariam Kobelo alisema baadhi ya wafanyabiashara wa SADC wameonyesha nia ya kutengeneza ubia na wafugaji wa asali Tanzania.

“Ziko nyingi lakini kwa SADC ni Afrika Kusini, lakini kuna nyingine Ethiopia, Uganda, Kenya na Rwanda zimeonyesha dhamira, wanataka kukutana na wafugaji ili watengeneze mtandao wa kuanza kusafirisha asali nchi kwao kwa njia ya ubia,” alisema Mariamu.

Kwa mujibu wa TFS, aina ya asali zinazozalishwa Tanzania ni asali inayotokana na miti ya miombo (Tabora), mitunduru (Shinyanga), Mikaratusi (Iringa), miti ya milimani (Kilwa), Vichaka vya Itigi (Manyoni) na Miti ya Mikoko (Ukanda wa Pwani).

Uzalishaji wa asali na nta unaingizia Serikali fedha za kigeni dola 1.7 milioni kila mwaka kupitia nguvu kazi ya watu milioni mbili walioajiriwa katika mnyororo wa thamani.

Pia Soma

Katika hatua nyingine, Mariamu ametoa wito kwa Watanzania kuingia katika fursa ya ufugaji wa nyuki kutokana na fursa nyingi zilizopo katika soko la SADC huku akiwataka kuachana na utamaduni wa kukata miti hovyo.

Aliwataka Watanzania pia kutangaza na kutumia utalii wa Misitu 17 ya hifadhi ya Mazingira Asilia.

Chanzo: mwananchi.co.tz