Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Angellah Kairuki anavyohakikisha wanawake wananufaika na madini

28116 Pic+kairuki TanzaniaWeb

Wed, 21 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ni mbunge wa viti maalumu kipindi cha pili tangu mwaka 2010. Huyu ni Angellah Kairuki.

Pamoja na majukumu yake serikalini, Kairuki anawajibika vyema katika Umoja wa Wanawake wa CCM Tanzania (UWT).

Hiki ndicho chombo kinachohusika na kupitisha majina ya wabunge hao, kabla ya uteuzi wao ndani ya chama haujathibitishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa.

Mwanamama huyu ameonyesha kuwajibika vilivyo katika nafasi za uongozi anazopewa tangu akiwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria na hivi karibuni kupanda hadi Waziri katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora na sasa Waziri wa Madini.

Naam, Kairuki ni Waziri wa Madini. Hii ni wizara nyeti na yenye changamoto lukuki, lakini tegemeo kwa nchi kutokana na mapato yatokanayo na madini.

Akiwa kwenye nafasi hiyo, anaeleza jinsi alivyoongeza mapato kwa kuongeza makusanyo yasiyo ya kodi ya madini.

Mathalan, anasema katika mwaka 2017/18 makadirio ya makusanyo yalikuwa Sh194.6 bilioni, chini yake wizara hiyo imepita lengo kwa asilimia 155 kwa kukusanya Sh301.2 bilioni.

“Mwaka 2018/19 makadirio ni Sh310 bilioni, lakini mimi kama waziri mwenye dhamana nataka tufike mbali zaidi ya hapo, yaani tuzidi makusanyo ya mwaka 2017/18,“ anasema Kairuki.

Pamoja na majukumu hayo, Kairuki hutumia muda mwingi kuwasaidia wanawake wenzake ili nao wapate mwangaza kwenye masuala ya kiuchumi na hasa katika sekta ya madini, kama anavyoeleza mwenyewe.

“Pamoja na kufanya mambo mengine na kushirikiana na watu wa jinsi ya kiume kwenye utendaji wa kila siku, shauku yangu ni kuona wanawake nao kama wanajamii wanashiriki vema kwenye sekta ya madini, ndiyo maana tuna mipango mingi kuhakikisha ushiriki wao ipasavyo,” anaeleza.

Kutokana na imani anasema amesaidia wanawake wachimbaji wa madini wa vikundi vya Tawoma, Wima na Miva kwa kuwapa ofisi zaidi ya 24 katika jengo la Shirika la Madini la Taifa (Stamico).

Anasema atatoa ofisi nyingine kwa wachimbaji wadogo wanawake kwenye jengo jipya wanalojenga katika Chuo cha Madini jijini Dodoma.

Anafafanua kuwa kupitia wizara yake amesimamia na kutoa leseni kwa wachimbaji wanawake 600, wakiwa ni mmojammoja na vikundi.

“Mbali na hayo wizara ninayoiongoza imetoa mikopo na ruzuku kwa zaidi ya vikundi 21 katika awamu ya kwanza na katika awamu ya pili tumetoa kwa vikundi 350, Saccos 15,”anasema.

Ili iwe rahisi kuwawezesha wanawake wengi zaidi, Kairuki anatoa wito wajiunge katika vikundi na milango ipo wazi.

Pamoja na kuwapatia ofisi, Waziri huyo anasema pia wizara yake ina mpango wa kuanzisha vituo saba vya mafunzo ya vitendo kwa wanawake kuhusu namna ya kuchimba na kuchenjua madini.

“Pia, taasisi ya Jeomolojia ya Arusha inatoa mafunzo ya kuongeza thamani ya madini kwa wanawake 83. Hapa wanajifunza ukataji, ung’arishaji, na mafunzo haya yapo kwenye vituo vingine ikiwamo Nachingwea na kile cha AMGC kilichopo Kunduchi, Dar es Salaam,” anasema.

Waziri Kairuki anasema kwa kuwatumia wanawake kwenye kazi ndogondogo za madini, kunapunguza ajira kwa watu wa nchi nyingine na kuzibakisha hapa nchini.

“Nina ushahidi kuna nchi (kwenye mabano) imepoteza ajira 15,000 baada ya kuanzisha programu za kuongeza thamani ya madini hapa nchini kwa kutumia wanawake,” anafafanua Kairuki.

Anasema Wizara yake pia inatenga maeneo maalumu kwa ajili ya wachimbaji wadogo, huku kipaumbele kikiwa ni kwa wanawake na vijana.

Lengo la kutoa mafunzo hayo, Waziri anasema ni kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu kwenye sekta ya madini kama ilivyo kwa wanaume.

Anasema sifa waliyonayo wanawake wana uwezo mkubwa wa kufanya kazi za mikono, hivyo inakuwa rahisi kwao kuongeza thamani ya madini.



Chanzo: mwananchi.co.tz