Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Alizeti kimbilio mbadala wa pamba kwa wakulima Geita

Alizeti.jfif Alizeti kimbilio mbadala wa pamba kwa wakulima Geita

Wed, 7 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kilimo cha pamba kina umuhimu mkubwa kwa Taifa, likiwa zao muhimu kibiashara linalotoa ajira kwa watu wengi kuanzia hatua za kilimo hadi usindikaji na masoko.

Hata hivyo, bei ya soko isiyotabirika, mabadiliko ya hali ya hewa na changamoto za upatikanaji wa viuatilifu, vimetajwa kuwa sababu kwa baadhi ya wakulima wilayani Geita kuhama kutoka kilimo cha pamba na kuanza kulima alizeti.

Halmashauri ya Mji wa Geita yenye wakulima waliosajiliwa 15,277 kati yao 7,009 wanalima alizeti, 2,611 wanalima pamba wakiwa ni pungufu kutoka 4,000 waliolima zao hilo katika msimu uliopita wa 2022/23.

Wakulima wengine wanalima mazao mbalimbali mchanganyiko.

Ofisa kilimo katika Halmashauri ya Mji wa Geita, Notkery Mwalongo akizungumza na Mwananchi Digital amesema baadhi ya wakulima wamekata tamaa kulima pamba kutokana na changamoto za bei.

“Wananchi wamekata tamaa kwa changamoto za bei, ndiyo maana unaona wengi wamekimbilia alizeti ambayo soko lake lipo na unauza wakati wowote, husubiri msimu, tofauti na pamba lazima kusubiri bei ya soko la dunia,” amesema Mwalongo.

Wapewa mbegu za alizeti

Akizungumzia msimu wa kilimo kwa mwaka 2022/23 amesema halmashauri hiyo kupitia fedha za uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR), ilitenga Sh50 milioni kwa ajili ya ununuzi wa mbegu bora za alizeti, lengo likiwa kuendeleza mnyororo wa thamani wa zao hilo.

“Ugawaji wa mbegu bure kwa wakulima umeweka hamasa kwa wananchi ambao walilima ekari 5,617 na kupunguza bei ya mafuta kutoka Sh9, 000 kwa lita hadi kufikia Sh5,000 inayouzwa hivi sasa madukani,” amesema Mwalongo.

Kutokana na wananchi kuchangamkia kilimo cha alizeti, baadhi ya taasisi zimeunga mkono jitihada hizo kwa kutoa mbegu bora.

Hivi karibuni akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi mbegu za alizeti kwa wakulima wa Kijiji cha Bunegezi, Kaimu Meneja Mwandamizi wa Mahusiano wa Kampuni ya Uchimbaji Dhahabu ya Geita (GGML), Elibariki Jambau amesema ugawaji wa mbegu ni jitihada za kampuni kuhakikisha wakulima wanaanza kuzalisha mazao ya biashara na kuleta tija, badala ya kutegemea mazao ya chakula pekee.

“Tumekuwa tukiwasaidia wakulima wa alizeti na mpunga kwa kuwapatia mbegu bora za alizeti, kuwajengea viwanda vya kuchakata na kuongeza thamani kwenye alizeti, pia kuwapatia trekta ya kulima mashamba yao, lengo ni kuwa na wakulima wanaojitegemea na wenye miradi endelevu hata baada ya GGML kumaliza shughuli za uwekezaji,” amesema Jambau.

Amesema GGML imetumia zaidi ya Sh300 milioni kwa ujenzi wa viwanda viwili vya kuchakata alizeti na ununuzi wa mbegu za zao hilo kilo 23,500 kwa ajili ya wakulima wa kata 13 za Halmashauri ya Mji wa Geita.

Viwanda hivyo vimejengwa katika kata za Bulela na Ihanamilo lengo likiwa ni kuwawezesha wakulima kupata zao mbadala la biashara na kuongeza kipato cha familia.

Mbali ya hilo, vitawapunguzia gharama za ununuzi wa mafuta kutoka nje ya mkoa.

Mkulima, Ikorongo Otto amesema kilimo cha alizeti hakina usumbufu kama ilivyo kwa pamba.

“Mkulima analima na kufanya palizi mara mbili, halazimiki kuweka dawa, tofauti na pamba inayomlazimu kupalilia mara nne na ni zao linaloshambuliwa na wadudu kwa wingi,” amesema.

“Alizeti haihitaji maji mengi na uzalishaji wake ni mkubwa, mkulima anapata mafuta lakini pia anauza mashudu kama chakula cha mifugo.”

Otto amesema awali walishindwa kulima alizeti kutokana na changamoto ya mbegu, lakini kwa miaka miwili sasa wamekuwa wakipata ufadhili kutoka GGML.

Mkulima katika Kijiji cha Bunegezi, George Kamanyilo amesema kilimo cha alizeti hakina gharama kubwa kwenye uzalishaji, pia mkulima anaweza kuvuna mara mbili kwa mwaka.

Kamanyilo amewashauri wananchi kutobaki kwenye zao moja la pamba, badala yake walime mazao tofauti ili kujipatia chakula na kipato.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live