Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Akaunti Jumuifu yaibua mshikemshike bungeni

10320 Akaunt+pic TZW

Sat, 30 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Baadhi ya wabunge wakiongozwa na Kamati ya Bajeti wametofautiana na Serikali kuhusu kufutwa kifungu cha 17A cha Sheria ya Sekta ya Korosho na kuanzisha Akaunti Jumuifu ya Hazina (TSA).

Pia wamepinga pendekezo la kufutwa Tume ya Mipango.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango akiwasilisha Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2018 alisema lengo la kufutwa kwa kifungu cha 17A ni kuyafanya makusanyo yanayotokana na ushuru wa mauzo ya korosho ghafi nje ya nchi kuwa sehemu ya mapato ya mfuko mkuu wa Serikali badala ya utaratibu wa sasa.

Alifafanua kuwa utaratibu wa sasa wa asilimia 65 ya mapato hayo ni sehemu ya mapato ya mfuko wa kuendeleza zao la korosho na uendeshaji wa Bodi ya Korosho.

Waziri Mpango alisema gharama hizo zitagharamiwa kupitia Bajeti ya Serikali chini ya usimamizi wa Wizara ya Kilimo kama inavyofanyika sasa kwa mazao mengine ikiwamo pamba, kahawa na pareto.

Hata hivyo, mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Hawa Ghasia alisema kamati yake inapendekeza sehemu ya nne ya muswada huo ifutwe.

Ghasia alisema kwa kuwa majukumu ya kuendeleza zao la korosho yamehamishiwa Bodi ya Korosho, kamati inapendekeza fedha kwa ajili ya kuendeleza zao hilo zipelekwe katika bodi hiyo kwa mgawanyo utakaokubalika kati ya Serikali na wadau wa korosho nchini.

“Kamati inapendekeza kufanya mabadiliko katika kifungu cha 5(1) cha Sheria ya Tasnia ya Korosho ili pamoja na mambo mengine, kuongeza jukumu kwa Bodi ya Korosho kusimamia uendelezaji wa zao la korosho,” alisema Ghasia.

Uanzishwaji wa TSA

Kuhusu uanzishwaji wa akaunti ya TSA, Waziri Mpango alisema anapendekeza marekebisho ya Sheria ya Fedha za Umma ili kuwezesha utekelezaji wa akaunti hiyo jumuifu itakayoanza Septemba.

Alisema uwepo wa akaunti hiyo pamoja na mambo mengine, utarahisisha usimamizi wa fedha za Serikali kwa kupunguza idadi ya akaunti kwenye benki za biashara na BoT, kupunguza gharama za kibenki zinazolipwa sasa na Serikali kufuatia huduma zinazotolewa kwa Serikali na benki za biashara.

Dk Mpango alisema uwepo wa akaunti hiyo pia utapunguza nakisi kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali kwani fedha zilizopo kwenye akaunti za amana zitajumuishwa kwenye ukokotoaji wa bakaa katika Mfuko wa Serikali, tofauti na utaratibu wa sasa ambao akaunti hizo hazijumuishwi katika ukokotoaji huo.

“Kupitia marekebisho haya, waziri mwenye dhamana na masuala ya fedha apewe dhamana ya kuandaa kanuni za kuwezesha utekelezaji wa akaunti Jumuifu ya Hazina ambayo itaanza kazi Septemba 30, 2018,” alisema Dk Mpango.

Hata hivyo, Ghasia alisema kamati inaliomba Bunge kutoa muda zaidi kwa Serikali na Kamati ya Bajeti ili kuliangalia suala hilo kwa undani kwa niaba ya Bunge ili kuhakikisha suala hilo linafanyiwa kazi kwa ufasaha na ufanisi.

“Kamati inaishauri Serikali kukamilisha mashauriano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuhusu suala hili. Kamati inapendekeza Serikali kufanya mabadiliko katika kifungu cha 11(D) ili kuweka sharti la kuwezesha utaratibu huu kuanza kutumika Desemba, 2018,” alisema Ghasia.

Tume ya Mipango

Waziri Mpango akizungumzia Tume ya Mipango alisema muswada huo unapendekeza pia kufutwa kwa tume hiyo ili kutekeleza muundo wa Serikali ya Awamu ya Tano kwa mujibu wa hati ya mgawanyo wa majukumu ya mawaziri.

Alisema kutokana na kufutwa kwa sheria hiyo; majukumu, mali, madeni, haki, mashauri mbalimbali na mikataba iliyokuwa inahusu Tume ya Mipango itahamishiwa Wizara ya Fedha na Mipango.

“Waziri wa Fedha na Mipango baada ya mashauriano na Ofisi ya Rais, anaweza kuhamishia kwa wizara, taasisi ya Serikali mali na madeni ya tume hii ambapo uhamisho huo wa mali na madeni utatangazwa kupitia gazeti la Serikali,” alisema.

Alisema watumishi waliokuwa Tume ya Mipango ambao watahitajika katika ofisi mbalimbali za umma, watahamishiwa katika ofisi hizo kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma na wataendelea na masilahi ambayo hayatakuwa chini ya masilahi waliyokuwa wakipata wakiwa Tume ya Mipango.

Pia, Waziri Mpango alisema muswada huo unapendekeza kurejesha msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye huduma ya ukodishaji wa ndege.

Hata hivyo, mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti Ghasia akitoa maoni ya kamati alisema, “Kamati ya Bajeti haikubaliani na mapendekezo ya Serikali ya kufuta Sheria ya Tume ya Mipango, Sura ya 314. Kamati, inaona pendekezo la kufuta sheria hii si sahihi kwa sababu uamuzi wa Serikali wa kuunganisha Tume ya Mipango na Wizara ya Fedha hauondoi umuhimu wa kutokuwepo kwa sheria hii.

“Endapo sheria hii itafutwa na ikaonekana tume hii kuhitajika kuwapo miaka ijayo italazimu Serikali kuja bungeni ili kutunga upya sheria hii.”

Zitto aungana na kamati

Akichangia muswada huo, Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) Zitto Kabwe alisema, “Hakuna zao lolote lenye export levy zaidi ya korosho. Tanzania hii ni zao moja tu lina export levy pamba haina export levy, kahawa haina export levy, tumbaku haina export levy na ninaomba hili lieleweke na kwa nini korosho.”

Alisema kodi hiyo ilianzishwa na wadau wa korosho wenyewe na haijaanzishwa na Serikali baada ya wadau kukaa katika mkutano wao wenyewe wakajadili jinsi ya kuboresha zaidi zao hilo kwa kutambua Serikali haina fedha.

Alisema wakulima wa korosho kupitia mkutano wao mkuu walianza kwa kukubaliana wawe wanakatwa asilimia tatu na sasa imefikia asilimia 65 ili asilimia 35 zielekezwe kwa Serikali, “Na fedha hizo asilimia 65 ni za wakulima na si za Serikali kama alivyosema AG (Dk Adelardus Kilangi) hapa juu ya kesi ile.”

Kauli hiyo ilimfanya Spika Job Ndugai kumuuliza Zitto, kama mfuko wa korosho haukuwa mali ya umma kwa nini makusanyo yao yalikuwa yakikusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Akitoa ufafanuzi zaidi, Zitto alisema, “Swali zuri kabisa, wadau walisema kati ya asilimia 100, asilimia 35 zitakuwa zinakwenda TRA kama malipo ya kuwakusanyia fedha kwa hiyo Mheshimiwa Spika, hizi asilimia 65 ni za kwao kuzichukua fedha hizi haiwezekani, tusiwe wakatili jamani kwa mambo ambayo wameomba wenyewe watozwe.”

Zitto alisema uamuzi wa Serikali kutaka kuanzisha Akaunti Jumuifu ya Hazina (TSA) ni uvunjifu wa Katiba na sheria za ukaguzi.

Alisema inakwenda kukiuka sheria ya ukaguzi wa Taifa kumpa mamlaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kukaguza akaunti hiyo lakini ni kinyume cha Katiba ya nchi hivyo kuliomba Bunge kutokuwa sehemu ya uvunjifu huo wa sheria na Katiba.

Mbunge wa Tandahimba (CUF), Katani Katani alisema, “Kwa nini wasichukuliwe hatua, wakurugenzi wa bodi na si kufuta mfuko wa korosho?” Katani alisema kama kuna tatizo kwa nini waliohusika na ubadhirifu wasipelekwe mahakamni kuliko kuwaumiza wakulima wote.

Mbunge wa Siha (CCM), Dk Godwin Mollel aliunga mkono ushuru wa mauzo ya korosho kuingizwa katika Mfuko Mkuu wa Serikali akisema wakulima wamefanya vizuri katika uzalishaji.

“Ukiangalia sera ya viwanda, tumegeuka ni shamba la wengine kupita kwa haya marekebisho inaenda kuondoa kuwa wazalishaji wa kati na itafanya kuanzishwa kwa viwanda vya korosho,” alisema Dk Mollel.

Alisema Daraja la Mkapa limejengwa kwa kutumia fedha zilizopatikana kupitia mapato ya kutoka katika maeneo mbalimbali na si fedha zinazotokana na korosho na kutaka wabunge kuunga mkono sheria hiyo.

“Tunaunga mkono mawazo haya, hayaendi kumnyang’anya pato, bali yanaenda kuondoa watu wa kati na wanaopinga kuanzishwa kwa viwanda vya kubangua korosho kwa sababu wataenda kuwalinda,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz