Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ajira sekta binafsi zaporomoka

85087 Pic+ajira Ajira sekta binafsi zaporomoka

Fri, 22 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati Rais wa zamani, Benjamin Mkapa akihofia ongezeko la vijana wasio na kazi, taarifa zilizotolewa na Shirika la Takwimu (NBS) zinaonyesha kuwa kuyumba kwa sekta binafsi kumechangia tatizo hilo kuwa kubwa.

Katika kitabu chake cha “My Life, My Purpose (Maisha Yangu, Kusudi Langu)” kilichozinduliwa mapema wiki iliyopita, Mkapa, ambaye aliongoza Serikali ya Awamu ya Tatu, anasema taswira za vijana wasio na kazi alizoziona mwaka 2015 zinamtia hofu kuhusu mustakabali wa nchi na kwamba suala la ajira litakuwa hoja kuu katika chaguzi zijazo.

Mkapa ameshauri kuwa ni lazima kutafutwe mkakati madhubuti wa kukabiliana na tatizo hilo kwa kuwa linazidi kukua kadri siku zinavyokwenda.

Katika takwimu za NBS zilizotolewa Agosti 14 kuhusu matokeo ya mwenendo wa hali ya soko la ajira nchini, ajira katika sekta binafsi zilipungua kutoka ajira 239,017 mwaka 2016/17 hadi ajira 137,054 mwaka 2017/18.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa ajira katika sekta binafsi zimekuwa zikipungua kuanzia mwaka 2013/14 hadi 2017/18. Mwaka 2013/14 kulikuwa na ajira 408,756 na mwaka uliofuatia (2014/15) zikapungua hadi 257,373 na mwaka 2015/16 zikashuka hadi ajira 195,002.

Mwaka 2016/17 kulikuwa na ongezeko kidogo hadi ajira 239,017 lakini mwaka uliofuatia zikashuka.

Ipo haja sasa kwa sekta ya ajira na sekta ya elimu kukaa pamoja kubainisha mahitaji ya mafunzo vyuoni na kushirikiana bega kwa bega na taasisi za elimu katika kuandaa programu za pamoja za mafunzo,” anasema Faraja Kristomus wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

“Lengo la kuwa na programu za ushirikiano huo ni kuhakikisha kuwa mafunzo ya nadharia yaende sambamba na mafunzo kwa vitendo.’’

Wakati Kristomus akihusisha tatizo hilo la ajira na ukosefu wa stadi zinazotakiwa kutoka kwa wahitimu wa vyuo, katika kipindi cha kuanzia mwaka 2016, kampuni nyingi binafsi zilijikuta zikilazimika kufunga biashara baada ya Serikali kuanza kufuatilia kwa karibu masuala ya kodi na taratibu nyingine, huku baadhi ya kandarasi kama za ujenzi zikikabidhiwa taasisi za umma.

Sekta ya huduma pia iliathirika kutokana na uamuzi wa serikali kuendesha shughuli zake kama mikutano, semina na warsha katika majengo au taasisi zake na hivyo kuathiri sekta binafsi.

Kwa habari zaidi soma hapa: Kitendawili cha ajira Tanzania

Chanzo: mwananchi.co.tz