Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ajira milioni 6.4 kuzalishwa ujenzi wa viwanda

Waziri Jafo Atoa Rai Ya Kulinda Na Kuutunza Muungano.jpeg Ajira milioni 6.4 kuzalishwa ujenzi wa viwanda

Fri, 16 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ajira milioni 6.4 zinatarajiwa kuzalishwa kupitia mpango wa miaka mitano wa ujenzi wa viwanda nchini uliotangazwa na Wizara ya Viwanda na Biashara.

Mpango huo umetangazwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo leo Alhamisi Agosti 15, 2024 ambapo utatekelezwa ndani ya miaka mitano (2025 hadi 2030).

“Jumla ya viwanda vidogo, vya kati na vikubwa 9,048 vinatarajiwa kujengwa chini ya mpango huo ambapo kila mwaka kutakuwa na ujenzi wa viwanda 1,508,”amesema.

Dk Jafo amesema zaidi ya ajira milioni moja za moja kwa moja zitazalishwa katika kipindi cha mpango huo, huku ajira milioni 5.4 zisizo za moja kwa moja zikitarajiwa kupatikana kwa muda wa miaka mitano.

Amesema katika utekelezaji wa mpango huo kila mkoa utahamasisha ujenzi wa viwanda 55 kila mwaka katika kipindi hicho kwa mchanganuo wa viwanda vikubwa vitano, vya kati 20 na vidogo vidogo sana 30.

Kwa mujibu wa Dk Jafo, sekta zitakazohusika katika ujenzi wa viwanda hivyo ni madini, kilimo, mifugo, uvuvi, nishati, mawasiliano, ujenzi, elimu, biashara za huduma na uzalishaji wa bidhaa.

Amewataja wahusika kuwa ni wizara, taasisi za Serikali wezeshi, vyombo vya habari, taasisi na kampuni binafsi, tawala za mikoa na serikali za mitaa.

“Kila mwaka kutafanyika tathmini ya utekelezaji wa mpango huo wa viwanda. Kwa mkoa uliofanya vizuri zaidi utazawadiwa kombe maalumu (samia industrial Award),”amesema.

Amesema na mshindi wa kila mwaka atapewa kipaumbele cha kwenda kufanya utalii wa ndani katika moja ya vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini.

Amesema lengo la motisha ni kufanya kila mikoa itakayoshinda kila mwaka ipate heshima na kutambuliwa kwa kazi kubwa ya kulitumikia Taifa la Tanzania.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) na mchumi, Dk Lutengano Mwinuka amesema mpango mkakati mzuri walioufanya katika kuongeza ajira, lakini ili upate mafanikio mazuri ni vyema Serikali ikaweka vivutio katika eneo hilo.

Amesema ardhi nchini kwa ajili ya kuanzisha viwanda na biashara imekuwa ikipatikana kwa gharama kubwa, tofauti na ardhi kwa ajili ya makazi.

Ameshauri kuwekwa kwa kivutio katika eneo hilo kwa mikoa kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya uanzishaji wa viwanda, ambapo wawekezaji watawekewa masharti ya muda wa kutakiwa kuanzisha viwanda.

“Wanaweza kupewa hata muda wa mwaka mmoja wasipoanzisha wananyang’anywa eneo. Hili litawavutia wengi kuwekeza katika ujenzi wa viwanda nchini,”amesema.

Ukubwa wa tatizo la ajira

Februari 3, 2023 Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi alisema asilimia 12.2 ya vijana nchini walio na umri wa kati ya miaka 15 hadi 35 hawana ajira.

Katambi aliyasema hayo bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Kisesa (CCM) Luhaga Mpina aliyehoji ni vijana wangapi nchini hawana ajira, na Serikali imejiandaaje kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.

Mwaka 2017, Serikali kupitia Tamisemi ilitoa agizo la kuutaka kila mkoa kujenga viwanda vidogo na vya kati vipatavyo 100 hadi kufikia Desemba mwaka 2018.

Hata hivyo, Machi 2018, Tamisemi ilitoa taarifa kuwa jumla ya viwanda 1,285 kati ya 2,600 sawa na asilimia 49.4 vilijengwa hadi kufikia mwezi huo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live