Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa kiwanda cha Sukari kilichopo Mbigiri kitachangia ongezeko la ajira kwa watanzania kwani kinatarajiwa kutoa fursa za ajira 11315 ambazo ni ajira za moja kwa moja na ajira sio za moja kwa moja pindi Kiwanda hiki kitakapokamilika.
Ameyasema hayo Septemba 19, 2023 wakati alipotembele utekelezaji na kukagua wa ujenzi wa Kiwanda cha Sukari kilichopo Mbigiri Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro ambapo ameitaka Bodi ya Mkulazi kuhakikisha Kiwanda hicho kinaanza uzalishaji Oktoba 2023.
Prof. Ndalichako amemshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia mazingira wezeshi ya Uwekezaji kwa wawekezaji ambapo uwekezaji wa kiwanda hicho umetatua changamoto za ajira nchini.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilosa ambaye amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Shaka Abdul Shaka amesema kuwa wataendelea kutoa ushirikiano mzuri na kusimamia kwa karibu ujenzi wa kiwanda hiki kwani kitasaidia kuinua uchumi wa wananchi wa Kilosa.
Awali akiwasilisha taarifa, Mtendaji Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Mkulazi Selestine Some amesema kuwa Kampuni inatarajia kuanza uzalishaji wa sukari mwezi Oktoba 2023 baada ya kukamilika kwa Kiwanda hiki Septemba 30 ,2023 na kinatarajiwa kuzalisha sukari kwa matumizi ya kawaida(Brown Sugar) na matumizi ya viwandani (Refined Sugar).
Vile vile Mhe. Prof. Joyce Ndalichako ametembelea mradi wa machinjio ya kisasa ya Nguru Hills Ranch uliopo wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro.
Waziri Ndalichako amemshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji nchini na kuongeza kuwa mradi huo unamanufaa makubwa kwa wananchi kwa kutengeneza ajira na kuongeza kipato kwa wafugaji.