Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ajali ya MV Nyerere yaahirisha maadhimisho ya Tanzanite

18887 Pic+tanzanite TanzaniaWeb

Mon, 24 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kutokana na ajali ya MV Nyerere, Tasisi ya Tanzanite Founder Foundation (Taffo) imeahirisha sherehe za maadhimisho ya 51 ya kugunduliwa kwa madini ya Tanzanite.

Maadhimisho hayo yalipangwa kufanyika jana yakihudhuriwa na mgunduzi wa madini hayo, Jumanne Ngoma.

Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Asha Ngoma amesema waliandaa sherehe kubwa lakini kutokana na msiba wa kitaifa uliopo wameona wazungumze na waandishi wa habari tu.

Asha alisema huu ni wakati sahihi wa kuitangazia dunia kuwa madini ya Tanzanite yanapatikana Tanzania badala ya kuacha nafasi hiyo kwa baadhi ya mataifa ambayo hufanya sherehe za kujiongezea soko kwa kuyatangaza kuwa yanatoka katika nchi zao.

“Kenya, India na China ndiyo wauzaji wakuu wa Tanzanite katika masoko makubwa ambayo ni Marekani na Bara la Asia lakini ukweli ni kwamba huo ni urithi wetu Watanzania. Tusiposema sisi watasema wao na watatunyang’anya asili yetu,” alisema Asha.

Kuhusu manufaa ya madini hayo na hatua zinazochukuliwa na Serikali kuyalinda, Asha alisema ujenzi wa ukuta ni hatua muhimu ya kuyatambua madini hayo na kuhakikisha thamani yake inalindwa.

“Hatua ya Serikali kumtambua rasmi mgunduzi wa madini hayo na kujenga ukuta wa kulinda madini ni hatua nzuri ya kuyaongezea thamani,” alisema Asha.

Asha alisema taasisi hiyo mwezi ujao inatarajia kufanya mkutano mkubwa wa wadau wa Tanzanite kujadili namna madini hayo yanavyoweza kuleta manufaa zaidi kwa Taifa.

Mgunduzi wa madini hayo, Mzee Ngoma alimshukuru Rais John Magufuli kwa kutambua mchango wake na kumpa fedha za matibabu na kusisitiza yeyote anayetaka kujua kuhusu uvumbuzi wa madini hayo amtafute.

Chanzo: mwananchi.co.tz