Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Airtel yasogeza mbele uuzaji wa hisa zake za awali London

24687 ARTEL+PIC TanzaniaWeb

Wed, 31 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kampuni ya Bharti Airtel imesogeza mbele kwa miezi sita mpango wake wa kuuza hisa zake za awali (IPO) katika Soko la Hisa London (LSE) nchini Uingereza.

Bharti Airtel yenye makao makuu nchini India, ina matawi katika mataifa 14 Afrika ikiwamo Airtel Tanzania. Nchini India, kampuni hiyo ni ya pili kwa kuhudumia wateja wengi zaidi wakati nchini inashika nafasi ya tatu ikiwa nyuma ya Vodacom na Tigo.

Ili kuimarisha operesheni zake Afrika, kampuni hiyo ilikusudia kuuza hisa zake zenye thamani ya Dola 8 bilioni (zaidi ya Sh1.76 trilioni) Machi mwakani.

Lakini kutokana na kinachoelezwa kuwa ni kutotabirika kwa mazingira ya biashara na uchumi wa mataifa mengi yanayoendelea, imelazimika kusogeza mbele mpango huo mpaka Septemba 2019.

“Mwanzo tulipanga kufanya IPO Machi 2019 lakini tumesogeza mbele kwa nusu mwaka,” inasomeka sehemu ya taarifa ya kampuni hiyo ambayo mmiliki wake mkubwa ni Shirika la Mawasiliano Singapore (Singapore Telecommunications).

Wiki iliyopita, Airtel Africa ilipata uwekezaji wa Dola 1.25 bilioni kutoka kwa wawekezaji wa kimataifa ikiwamo kampuni ya Warburg Pincus, Temasek Holdings na SoftBank Group Corp.

Licha ya kuimarisha operesheni zake, fedha zitokanazo na mauzo ya hisa hizo zinakusudiwa kutumika kulipa deni la kampuni hiyo linalokadiliwa kuwa Dola 5 bilioni.

“Mpango wa kuuza hisa bado upo palepale na maandalizi yake yanaendelea vizuri,” inasomeka taarifa hiyo.

 

 

 

Chanzo: mwananchi.co.tz