Kampuni ya Airtel imepandishwa kizimbani ikidaiwa fidia ya Sh490 milioni kwa kuitumia sauti ya Nixon Bandago Haule kwenye tangazo la ‘Airtel the Smartphone Network.’
Kesi hiyo imefunguliwa na Haule Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam anayedai sauti inayosikika katika kaulimbiu hiyo na kutumika katika matangazo ya kibiashara ya Airtel ni yake lakini hakutoa ridhaa itumike.
Kwa mujibu wa hati ya madai, kiapo na nyaraka nyingine alizoziwasilisha mahakamani, Bandago anadai kuwa aliingia makubaliano ya awali na ofisa wa Airtel aitwaye Arnold Madale Oktoba mosi mwaka 2017 na baada ya kurekodi sauti aliambiwa asubiri iidhinishwe na menejimenti ili wasaini mkataba jinsi itakavyotumika, muda na haki nyinginezo anazostahili.
Katika hali ya kushangaza, anasema alianza kuisikia kaulimbiu hiyo yenye sauti yake katika vituo vya redio na runinga bila makubaliano yoyote kufanyika hivyo anaiomba mahakama iamuru kuwa mdaiwa alivunja hakimiliki zake.
Sh490 milioni za fidia anayoiomba zinajumuisha Sh390 milioni za hasara aliyoipata kwa ukiukaji huo wa haki miliki na Sh100 milioni kama riba.
Katika majibu yake, Airtel imekana kuwa na mkataba naye wa kutengeneza tangazo hilo isipokuwa ina mkataba na kampuni ya Oglivy Tanzania Limited tangu Novemba 18 mwaka 2015 kwa shughuli zote za masoko na matangazo ya kibiashara kwenye vyombo vya habari.
Airtel imesema Mandago aliingia mkataba na kampuni ya Oglivy Mei 10 mwaka 2018 na akaridhia sauti yake kutumiwa na Oglivy na au wadau wake kwenye matangazo yake na katika kampeni zake za kibiashara kwa malipo ya Sh600,000 jambo ambalo Mandago anasisitiza alikuwa ofisa wa Airtel.