Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Airtel hatihati kuorodheshwa kwenye Soko la Hisa Dar es Salaam

13592 Pic+arrtel TanzaniaWeb

Fri, 24 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Licha ya kuwasilisha waraka wa matarajio (prospectus) kuomba kuuza hisa za awali (IPO) kwenye Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE), kampuni ya Airtel imeendelea kupata hasara hivyo kujiweka kwenye nafasi ya kukosa sifa za kusajiliwa.

Taarifa za fedha za Bharti Airtel, kampuni mama ya Airtel Tanzania kwa mwaka 2017 zinaonyesha hasara ya kampuni hiyo ya tatu kwa idadi kubwa ya wateja nchini ilipungua kutoka Dola 56.4 milioni za Marekani (zaidi ya Sh127 bilioni) iliyopata mwaka 2016 mpaka Dola 48.06 milioni (zaidi ya Sh108 bilioni) mwaka jana.

Licha ya hasara hiyo, madeni ya Airtel ni makubwa kuliko mali ilizonazo. Kampuni hiyo inadaiwa kiasi cha Dola635.38 milioni (zaidi ya Sh1.43 trilioni) wakati mali zake zina thamani ya Dola233.96 milioni (zaidi ya Sh526.4 bilioni).

Pamoja na mambo mengine yaliyochangia hasara ya kampuni hiyo ni kushuka kwa mapato. Taarifa zinaonyesha mapato yalishuka mpaka Dola214.49 milioni kutoka Dola228.02 milioni (zaidi ya Sh513 bilioni) ilizopata mwaka juzi.

“Mpaka Desemba 2017, kampuni hiyo ilikuwa na hasara jumuishi inayofika Dola423.18 milioni (zaidi ya Sh952 bilioni) kutoka Dola357.16 milioni (zaidi ya Sh803.6 bilioni) za 2016. Operesheni za kampuni hiyo zinaendelea kutegemea zaidi fedha kutoka kampuni mama,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Ili kutekeleza Sheria ya Kiektroniki na Huduma za Posta (Epoka), Airtel yenye zaidi ya wateja milioni 10.6 iliwasilisha waraka wa matarajio kwa Mamlaka ya Masoko ya Hisa na Mitaji (CMSA) mwaka jana. Kwa mujibu wa vigezo vya CMSA, kabla ya kampuni yoyote kusajiliwa katika soko la hisa, pamoja na mambo mengine inapaswa kuwa na rekodi ya faida walau kwa miaka miwili mfululizo.

Hata hivyo, msemaji wa CMSA, Charles Shirima alisema hicho si kigezo pekee kinachozingatiwa zaidi na mamlaka hiyo kwa kampuni zinazotaka kusajili hisa zake sokoni.

“Zipo kampuni zinazopata hasara lakini zinaruhusiwa kuorodheshwa kwa sharti kwamba hazitatoa gawio kwa miaka miwili au mitatu ya kwanza. Hizi ni zile ambazo huonekana ni (muhimu zaidi) more potential,” alisema Shirima.

Kwenye waraka wake ambao bado haujaridhiwa na CMSA, Airtel inatarajia kupata mtaji wa Dola11.02 milioni (zaidi ya Sh24.8 bilioni) kutokana na mauzo ya asilimia 25 ya hisa zake.

Sheria ya Epoca inazitaka kampuni za mawasiliano nchini kuorodhesha walau asilimia 25 ya hisa ili kuwapa fursa Watanzania kuwa sehemu ya wamiliki. Ingawa utekelezaji ulipaswa kukamilika Juni mwaka jana, ni Vodacom pekee ilitekeleza baada ya kukidhi vigezo.

Ili kuboresha huduma zake, kampuni hiyo ilikopa Dola4.58 milioni (zaidi ya Sh10.3 bilioni) mwaka jana ingawa mapato yatokanayo na kupiga simu yalishuka kutoka Dola102.6 milioni (zaidi ya Sh230.9 bilioni) za mwaka 2016 hadi Dola82.9 milioni (zaidi ya Sh186.5 bilioni).

Mkopo huo ulichangia ongezeko la madeni ya kampuni hiyo kutoka Dola449.07 milioni (zaidi ya Sh1.01 trilioni) mpaka Dola477.37 milioni (zaidi ya Sh1.07 trilioni) ndani ya kipindi hicho.

Ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, kampuni hiyo ilipata hasara Kenya pia, lakini ikaongezea faida yake kwa takriban asilimia 30 nchini Uganda.

Wakati faida yake ikiongezeka kutoka Dola44.9 milioni mpaka Dola 62.12 milioni nchini Uganda, hali ilikuwa tofauti Kenya ambako Airtel ilipata hasara ya Dola59.5 milioni ikipungua kutoka hasara ya Dola79.4 milioni iliyopata mwaka 2016.

Chanzo: mwananchi.co.tz