Huenda ahueni ya bei ya sukari ikaanza kuonekana siku zijazo baada ya Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), kutangaza kuanza kuingia nchini kwa shehena ya sukari waliyokuwa wameagiza nje ya nchi.
Pia viwanda ambavyo vilikuwa vimesitisha uzalishaji kutokana na mvua za El-nino vimeombwa kurejesha huduma ili kukabiliana na uhaba huo.
Sukari iliyoagizwa itaanza kuingia nchini kati ya Januari 22 na 23 mwaka huu, huku ikitajwa kwenda kurejesha bei katika hali iliyokuwapo awali ambayo si zaidi ya Sh3000.
Bodi hiyo pia imewakemea watu wanaotumia vibaya uhaba wa bidhaa hiyo na kupandisha bei hadi kufikia kati ya Sh4000 hadi Sh6000 kwa baadhi ya mikoa, ikitangaza kuwachukulia hatua.
Akizungumza na wandishi wa habari jana jijini hapa Mkurugenzi wa SBT, Profesa Kenneth Bengesi alisema sukari hiyo itaingia kwa viwango tofauti kwa lengo la kuleta ahueni kwa wananchi.
Sukari hiyo ni kati ya tani 50,000 zilizokuwa zimeagizwa na Serikali kupitia kibali kilichotolewa mwishoni mwa mwaka jana.
Alisema kwa kawaida, vibali vya uagizaji sukari hutolewa kuanzia Machi wakati viwanda vingi vinafunga shughuli zake kwa ajili ya matengenezo, lakini mwaka jana hatua hiyo ilifanyika ili kuleta ahueni kwa wananchi.
Uhaba wa sukari nchini unatajwa kuchangiwa na kuwapo kwa changamoto mbalimbali ikiwemo mvua za El nino zilizoweka ugumu katika uzalishaji kutokana na kuharibika kwa miundombinu, mashamba kujaa maji jambo ambalo lilifanya miwa kupoteza sukari nyingi.
Hali hiyo ilifanya uzalishaji wa sukari kushuka kwani kiwango kilichokuwa kikipatikana katika miwa kilikua kidogo ikilinganishwa na uzalishaji ambao unafanyika bila kuwapo kwa hali hiyo ya mvua.
Changamoto hizo zilifanya lengo lililokuwa limewekwa awali la kuzalisha tani zaidi ya 550,000 kushindwa kufikiwa na badala yake tani 355,000 pekee ndiyo zikazalishwa.
"Kwa matarajio ya awali nchi ingekuwa na akiba ya tani zaidi ya 30,000 kwani mahitaji yetu yalikuwa tani 520,000," alisema Profesa Bengesi. Alisema mbali na kuingia kwa sukari hiyo pia Serikali ilikaa na viwanda vinavyoizalisha nchini na kuviomba kuendelea kufanya uzalishaji licha ya mazingira yaliyopo.
"Hili linaweza kufanya uzalishaji usiwe kwa kiasi kile kilichokusudiwa lakini kiwango kidogo kitakachopatikana kikiingizwa sokoni kitapunguza makali," alisema Profesa Bengesi.
Akizungumzia suala hilo, Msemaji wa Bakhresa Group, Hussein Sufian alisema, “Tulikaa nao, tukawapa mahitaji yetu na wanatusaidia hivyo uzalishaji unaendelea.
Hata hivyo, uzalishaji unaweza kuongezeka zaidi kati ya mwaka 2026/2027 baada ya viwanda vingine viwili vya sukari kuanza kujengwa nchini, kimoja kikiwa wilayani Rufiji mkoani Pwani na kingine wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.
Kiwanda cha Rufiji kipo hatua ya kuandaa mashamba ya miwa na ujenzi wake utaanza muda wowote, huku cha Kasulu kikiwa katika hatua ya kuangusha misitu ili waandae mashamba. Kwa pamoja vitaanza kazi mwaka 2026/2027.
Alisema kama nchi itahakikisha inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuongeza uzalishaji sukari kwa sababu njia ya uagizaji imekuwa ikiligharimu Taifa zaidi ya Sh350 bilioni ili kuziba pengo linapotokea.
Kabla ya hatua hizi kuchukuliwa bei ya sukari ilifika hadi Sh5,000 katika baadhi ya maeneo nchini jambo ambalo lilifanya vilio kuongezeka zaidi.
Justin Mpauka mmoja wa wafanyabiashara alisema sukari itakapokuwa nyingi kuzidi mahitaji itafanya bei ishuke. "Inaweza kuchukua siku kadhaa hali kurejea kama kawaida, na kuna wengine watapata hasara kama walinunua kwa bei ya jumla kubwa,kwani ikiongeza kwa hofu ya kukosa wateja watashusha bei," alisema Mpauka.
Tatizo ni la muda
Hiki kinachoshuhudiwa sasa kwa mujibu wa Profesa Bengesi, Tanzania haikuwahi kujitosheleza katika sukari tangu uuru.
Alisema hata Serikali ilipoanza ubinafsishaji mwaka 1998 kwa kuchukua kiwanda cha Kagera, Mtibwa, TPC na Kilombero bado uzalishaji ulikuwa chini. ubinafsishwaji afanyika tani 110,000 zilikuwa zinazalishwa huku mahitaji yakiwa ni tani 300,000 ambayo ni sawa na uhaba wa tani 190,000," alisema Profesa Bengeni.
Hadi mwaka 2016/2017 nchi ilikuwa ikiagiza tani 133,000 lakini mwaka 2017/18 Serikali iliamua kuchukua hatua za makusudi kuangalia namna ya kumaliza tatizo la sukari nchini na kuondokana na kutegemea bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi.