Bodi ya wakurugenzi ya Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) imeidhinisha dola za Marekani bilioni 1.5 (shilingi trilioni 3.48 za Tanzania) ziwezeshe uzalishaji wa chakula barani Afrika.
Rais wa AfDB, Dk Akinwumi Adesina, jana alitumia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa twitter kueleza kuwa fedha hizo zitasaidia wakulima milioni 20 wazalishe tani milioni 38 za chakula.
Dk Adeseina alijivunia AfDB kutoa fedha hizo na akaeleza kuwa Afrika inahitaji mbegu ili kujitosheleza kwa chakula.
Taarifa ya benki hiyo ilieleza kuwa kutokana na athari za vita ya Urusi na Ukraine hivi sasa Afrika inakabiliwa na upungufu wa takribani tani milioni 30 za chakula hasa ngano, mahindi, na maharage ya soya mazao ambayo huletwa kutoka katika nchi hizo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, fedha zilizotolewa zitawezesha wakulima wadogo kuziba pengo la upungufu wa chakula na kwamba, wakulima barani humu wanahitaji mbegu bora na pembejeo za kilimo kabla ya kuanza kwa msimu wa kilimo.
Ilieleza kuwa fedha hizo zitawezesha wakulima wadogo milioni 20 kupata mbegu na mbolea.
Taarifa ya AfDB ilimkariri Dk Adesina akisema misaada ya chakula haiwezi kuitosheleza Afrika na kwamba wakulima wanahitaji zana za kisasa na kwamba Afrika itajilisha yenyewe.
Dk Adesina alisema mawaziri wa fedha na kilimo Afrika walikubaliana kutekeleza mageuzi kukabili vikwazo vya ufanisi wa masoko ya zana za kisasa za kilimo.
Alisema tangu kuanza kwa vita ya Urusi na Ukraine bei ya ngano Afrika imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 45 na bei ya mbolea imeongezeka kwa asilimia 300.
Dk Adesina alisema Afrika inakabiliwa na upungufu wa tani milioni mbili za mbolea, nchi nyingi za Afrika tayari zimekumbwa na ongezeko la bei za mikate na bidhaa nyingine za vyakula.
Alisema kama upungufu wa mbolea utaendelea uzalishaji chakula Afrika utapungua kwa asilimia 20 na bara hili litakosa zaidia ya dola za Marekani bilioni 11.
Taarifa ya AfDB ilieleza kuwa fedha walizotoa zitawezesha uzalishaji wa tani milioni 11 za ngano, tani milioni 18 za mahindi, tani milioni sita za mchele, na tani milioni 2.5 za maharage ya soya.