Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

AfDB yatoa bilioni 289/- mradi wa maji Dodoma

2db17e0ecbef97a7696a5d914a37f45b AfDB imekua mdau mkubwa wa maendeleo nchini

Tue, 17 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imetoa mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 125.2 sawa na Sh bilioni 289.34 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa maji safi na usafi wa mazingira Dodoma.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alisaini mkataba huo Dar es Salaam kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Mwakilishi Mkazi wa AfDB, Dk Patricia Laverley.

Dk Mwigulu alisema mradi huo unaokadiriwa kuwanufaisha zaidi ya wakazi milioni mbili, utasaidia kutatua changamoto ya upungufu wa maji katika Jiji la Dodoma na wilaya za Bahi, Chemba na Chamwino “Mradi huu umesubiriwa kwa muda mrefu na wananchi wa Dodoma, lakini pia ni mradi ambao Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anatamani kuona unatekelezwa.

Kusainiwa kwa mkataba wa mkopo huu kutaleta manufaa makubwa kwa wananchi na upatikanaji wa maji ya uhakika kwa ajili ya matumizi ya viwandani,” alisema Dk Mwigulu.

Alisema mradi huo utatekelezwa kwa miaka mitano na utahusisha ujenzi wa Bwawa la Maji la Farkwa lenye uwezo wa kuhifadhi maji mita za ujazo 470, ujenzi wa mitambo ya kusafisha na kutibu maji yenye uwezo wa kuzalisha mita za ujazo 128,000 kwa siku na mambo mengine.

Dk Mwigulu aliiomba AfDB iangalie uwezekano wa kufikisha mradi huo kwenye maeneo mengine jirani na eneo la mradi ukiwamo Mkoa wa Singida.

“Mnapoanza utekelezaji wa mradi huu mkubwa muangalie pia maeneo jirani; mfano ukifika Bahi pembeni kidogo kuna Manyoni Mashariki ambayo kuna shida kubwa ya maji na kuna mafuriko ya mara kwa mara, Kongwa kunapopakana na Chemba na Chamwino kuna shida kubwa ya maji pia, hivyo ni vyema kuyahusisha maeneo hayo kwenye mradi,” alisema.

Alisema Rais Samia ameagiza miradi yote ya maji itakayotekelezwa nchini kuanzia sasa iweze kuzalisha maji ya matumizi ya majumbani na kusaidia shughuli nyingine za uzalishaji kama vile kilimo, mifugo, uvuvi ili kuimarisha ustawi wa jamii kwa kujipatia kipato.

Alirudia maombi ya serikali kwa AfDB itoe mkopo wenye masharti nafuu kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) utakaoziunganisha na nchi jirani za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Dk Laverley alisema AfDB ipo tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania kutekeleza mradi huo wa maji Dodoma na kusaidia utekelezaji wa miradi mingine.

Alisema mkopo huo wenye masharti nafuu wenye thamani ya dola za Marekani milioni 125.2 umefikisha kiasi cha fedha kilichowekezwa na benki hiyo nchini kufikia dola za Marekani bilioni 2.5 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 23 ya maendeleo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live