Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

AfDB yaikopesha Tanzania Sh589 bilioni

44973 Mkpopic AfDB yaikopesha Tanzania Sh589 bilioni

Wed, 6 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imetia saini mikataba miwili ya mkopo wa Sh589.26 bilioni na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa barabara ya Kabingo, Kakonko Kasulu na Manyovu mkoani Kigoma yenye urefu wa kilomita 260.

Utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa barabara hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya awamu ya tano unaolenga kuimarisha miundombinu ya usafiri ili kuchochea kasi ya maendeleo ya uchumi wa viwanda na jamii kwa ujumla.

Akizungumza wakati wa utilianaji wa saini wa mikataba hiyo leo Jumanne Machi 5, 2019 jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James amesema mradi huo utawaondolea adha ya usafiri ya muda mrefu wakazi wa Kigoma na kufungua milango ya maendeleo ya kiuchumi na kusaidia kuimarika kwa ushirikiano wa kikanda wa nchi za Afrika Mashariki.

"Barabara ya Kabingo-Kasulu na Manyovu ni kiunganishi muhimu katika maendeleo na uboreshaji wa biashara ndani na nje ya nchi.”

“Mradi huu pia utakwenda sambamba na ujenzi wa Barabara ya Rumange -Gitazi yenye urefu wa kilomita tano nchini Burundi, yote hii ni kuboresha mtandao wa barabara za Afrika," amesema.

Amesema mbali na kuleta maendeleo ya kiuchumi pia utekelezaji wa mradi huo utapunguza adha ya usafiri na gharama za utengenezaji wa magari na kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii.

"Kwa muda mrefu Kigoma imekuwa nyuma kimaendeleo. Kupitia mradi huu tunaenda kuifungua Kigoma katika uchumi na maendeleo na ikumbukwe fedha hizi ni za mkopo wenye masharti nafuu ambao utalipwa ndani ya miaka 30 hadi 40," amesema.

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa AfDB, Alex Mubiru amesema benki hiyo itaendelea kuchangia shughuli za maendeleo kwa Tanzania na kwamba imeguswa na hali ya changamoto ya usafiri mkoani Kigoma ndiyo maana imetoa fedha hizo.

"Mkataba wa kusaini fedha hizi ni moja ya mIkakati ya Benki kuisaidia Serikali ya Tanzania katika kuboresha miundombinu ya barabara ili kukuza uchumi wa nchi," amesema Mubiru.



Chanzo: mwananchi.co.tz