Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Abiria waliokata tiketi Fastjet wasotea nauli

33903 Pic+fastjet Tanzania Web Photo

Sat, 29 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wateja wa Shirika la Ndege la Fastjet ambalo shughuli zake zimesimamishwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), wanaendelea kusotea marejesho ya nauli zao hususani ambao walinunua kwa kutumia mifumo ya kielektroniki.

Jana, Mwananchi lilifika katika ofisi za Fastjet zilizopo Mtaa wa Samora na Barabara ya Julius Nyerere jijini hapa na kukuta baadhi ya wateja wakifuatilia kurudishiwa fedha zao wakiwamo waliokuwa wamefika katika ofisi hizo kwa mara ya nne bila mafanikio.

Watoa huduma wa ofisi hizo walikuwa wakiwaambia wateja waliofika kuwa kuna tatizo la kimtandao, lakini fedha zao zitarejeshwa mapema.

Lakini kwa wale waliolipia kwa fedha taslimu waliambiwa wakienda kwenye ofisi zilizopo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), watalipwa haraka zaidi na hata kama fedha zitakuwa zimekwisha kesho watapata.

“Inaonekana hawana fedha, lakini wanashindwa kutuambia ukweli. Mimi nililipa kwa M-pesa, tarehe 22 mwezi huu nilikamilisha taratibu zote na wakaniambia fedha zangu zitarejeshwa wakati wowote, hadi leo hazijarejeshwa, nimekuja mara ya tatu kufuatilia,” alisema Atanus Sospeter, mteja wa shirika hilo aliyekutwa katika ofisi za Mtaa wa Samora.

Sospeter ambaye alitaka kusafiri Desemba 16, alisema baada ya safari hiyo kuahirishwa aliamua kutafuta usafiri mbadala na anadai Sh206,000 alizolipia tiketi ya kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza.

Abiria mwingine, Josephat Mbula alisema baada ya shirika hilo kuzuiwa kufanya shughuli zake walimwahidi kuwa angepatiwa tiketi nyingine ya kusafiri siku nyingine, lakini hadi jana hawajafanya hivyo.

“Mwanzo walisema watanipa tiketi nyingine, kwa kuwa nilikuwa bado niko likizo nilikubali, lakini mpaka likizo yangu inakaribia kwisha sijapatiwa tiketi wala fedha ambazo ningeweza kutafutia usafiri mwingine wa kunifikisha Mwanza kwenye kituo changu cha kazi,” alisema Mbula.

Katika mahojiano na gazeti hili Desemba 26, Mwenyekiti Mtendaji wa Fastjet, Lawrence Masha alisema tayari shirika hilo limewarejeshea fedha baadhi ya abiria, lakini limeishiwa pesa kwa kuwa lilikodi ndege na kugharamia mambo mengine ili kurejesha huduma.

Masha alisema kipaumbele cha shirika hilo ni kuwasafirisha abiria na siyo kuwarudishia fedha.

Hata hivyo, juzi, wakati Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) ikikanusha taarifa za Masha kuzuiwa kuingiza ndege zake nchini ilisema itahakikisha kila mtu anayeidai Fastjet anapata fedha zake.

Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari aliliagiza shirika hilo kuwasilisha orodha ya abiria ambao wamelipwa na ambao hawajalipwa likiambatanisha na mpango wa namna ya kuwalipa.



Chanzo: mwananchi.co.tz