Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ATCL yazindua safari Chato -Dar es Salaam

C3eabef4c8b2688a7437b217a3922bae.jpeg ATCL yazindua safari Chato -Dar es Salaam

Tue, 5 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

KAMPUNI ya Ndege Tanzania (ATCL) imezindua safari kutoka Uwanja wa Ndege wa Chato mkoani Geita hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Ladislaus Matindi alizindua safari hizo jana na kubainisha kuwa, zinatarajiwa kuanza rasmi Januari 9 mwakani na kutakuwa na safari mbili kwa wiki kwa siku za Alhamisi na Jumamosi. Matindi aliwaeleza waandishi wa habari kuwa, kuanza kwa safari hizo kunatimiza azma ya ATCL kufikisha huduma kila eneo la nchini.

"Kuanzisha safari hizi tumeangalia mambo mengi ikiwemo uwezo wa uwanja wa ndege ambao una kilometa tatu ambazo zinakidhi kigezo cha kupokea ndege kubwa zikiwemo airbus na dreamliners,” alisema.

Matindi alisema safari hizo zitawapunguzia wananchi wakiwemo wafanyabiashara wa Geita tatizo la kutembea zaidi ya kilometa 200 kwenda Mwanza na Bukoba kufuata huduma hiyo.

"Pia tumelenga kukuza sekta ya utalii kwani uwanja upo karibu na hifadhi za Burigi Chato na Rubondo na tumelenga abiria wa nchi jirani za Burundi, Rwanda na Uganda ambao ni majirani zetu, kwani baadaye tumenuia kufanya safari zetu mara tatu kwa wiki kutokea Chato kupitia Kahama na Mwanza hadi Dar es Salaam," alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel alisema safari hizo zitaongeza fursa na kuchagiza maendeleo ya kiuchumi. Aliyakaribisha mashirika mengine ya ndege ndani na nje ya nchi kuanzisha safari kutokea uwanja huo kwani mkoa una miundombinu rafiki kupokea wageni kutoka mataifa yote.

Mbunge wa Chato ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani aliihakikishia ATCL kuutunza uwanja huo ili safari hizo ziwe endelevu. Dk Kalemani aliwashauri ATCL waangalie uwezekano wa kufanya safari kutoka Chato kwenda viwanja vya Kilimanjaro na Dodoma kwa kuwa ni mikoa yenye abiria wengi kwa sasa.

Chanzo: habarileo.co.tz