Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ATCL yashirikiana kibiashara kimataifa na kampuni saba za ndege

Atcl Pc Data ATCL yashirikiana kibiashara kimataifa na kampuni saba za ndege

Thu, 8 Sep 2022 Chanzo: Habarileo

Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) imesema inashirikiana kibiashara na kampuni saba za ndege za kimataifa.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi alisema hayo wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ilipopokea, kujadili na kushauri baada ya kupata taarifa ya utendaji wa ATCL na Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA).

Matindi alizitaja kampuni hizo kuwa ni Qatar Airways, Air India, Emirates, KLM, Omani Air, Rwanda Air na Ethiopian Airlines.

Alisema ushirikiano huo umelenga kuhakikisha kuunganishwa kwa safari kwa abiria wa ATCL na mashirika hayo katika maeneo ambayo ATCL haifanyi safari zake.

Matindi pia alisema ATCL imeongeza vituo na kufanya mtandao wa safari kufikia vituo 26 vikiwemo 15 vya ndani na tisa vya nje.

Alivitaja vituo vya ndani ni Arusha, Bukoba, Dar es Salaam, Dodoma, Geita, Iringa, Kilimanjaro, Kigoma, Mbeya, Mpanda, Mwanza, Mtwara, Songea, Tabora na Zanzibar.

Vituo vya nje ni Bujumbura, Entebbe, Hahaya, Harare, Lusaka, Ndola, Nairobi, Johannesburg na Lubumbashi na vituo viwili vya nje ya Afrika, Mumbai – India na Guangzhuo – China.

Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari alisema mamlaka hiyo imesaini upya mkataba wa usafiri wa anga kati yake na nchi nyingine ili kufungua soko la usafiri huo kwa kuvutia mashirika mengine kutoa huduma nchini na kuimarisha ushindani katika utoaji wa huduma za usafiri wa anga nchini.

Hamza alisema TCAA imetoa leseni mpya 1,223 na kuhuisha leseni 270 katika fani mbalimbali katika Sekta ya usafiri wa anga.

Kamati hiyo iliishauri serikali kuiwezesha ATCL na kuiwekea mazingira rafiki ya kujiendesha kwa kuweka watendaji wenye mtazamo wa kibiashara.

“Serikali wekezeni zaidi katika Kampuni ya ATCL ili iweze kufanya vizuri zaidi kibiashara na isaidieni kumaliza madeni yaliyokuwepo kipindi cha nyuma,” alisema Mwenyekiti wa kamati hiyo, Seleman Kakoso.

Kamati hiyo pia iliishauri serikali iendelee kusimamia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) na kuboresha viwanja vya ndege vinavyoendelea kujengwa ikiwemo vya Iringa na Musoma na kusisitiza kasi katika ujenzi wake.

“Simamieni kwa karibu ujenzi wa viwanja vya ndege hapa nchini ili kuiwezesha ATCL kufanya vizuri kwa kuwa ufanisi wa kampuni hiyo unahitaji ubora wa viwanja vya ndege nchini,” alisema Kakoso.

Chanzo: Habarileo