Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ATCL yaruka ndani kwa asilimia 90

15cb4b71868dc7010890171be69b779b ATCL yaruka ndani kwa asilimia 90

Sun, 3 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MKURUGENZI Mkuu wa Kampuni ya Ndege Tanzania. (ATCL), Ladislaus Matindi, amesema kwa sasa ATCL imefanikiwa kurudisha miruko kwa soko la ndani kwa zaidi ya asilimia 90 baada ya kushuka hadi kufikia asilimia 80 kipindi cha Covid-19 huku ikitawala soko la ndani kwa asilimia 70.

Aliyasema hayo jana alipozungumza na Habari Leo kwa njia ya simu.

Matindi alisema katika wiki ya kwanza ya mwezi Januari mwakani, ATCL itaanza kufanya safari za kwenda Chato mkoani Geita na mwishoni mwa mwezi Februari au mwanzoni mwa mwezi Machi, ndege hizo zitaanza safari za kwenda Arusha, Songea na Mbeya.

Baadaye zitafuata safari za kwenda Lubumbashi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Nairobi nchini Kenya.

Matindi alisema mwaka huu ulikuwa na changamoto kubwa, siyo tu kwa ATCL, bali kwa sekta yote ya usafiri wa anga kutokana na janga la ugonjwa wa Covid-19.

Alisema kuenea kwa Covid-19 na masharti yaliyokuwepo ya kujikinga na kupunguza maambukizi, yalisababisha hali ya kibiashara ya ATCL kushuka hasa katika kipindi cha kuanzia mwezi Machi, ambapo walisitisha safari zote za kimataifa na pia kupunguza safari za ndani.

“Kwa hiyo unaweza ukaona kuna upungufu mkubwa kwa upande wa mapato, kuna upungufu mkubwa upande wa abiria, lakini tulijitahidi kutafuta njia zingine za kuhakikisha kwamba kampuni yetu inaendelea kufanya kazi na kupata mapato, pia tunaishukuru Serikali na hasa Rais John Magufuli ambaye alitusaidia sana kupata vibali vya kufanya safari za uokoaji,”alisema Matindi.

Alisema safari hizo za uokoaji, zilihusu kuwachukua abiria wa mataifa mengine na Watanzania waliotaka kurudi au kuja hapa Tanzania kutoka nchi za India, China, Madagascar, Ethiopia na mataifa mengine na kupeleka abiria katika mataifa hayo. Matindi alisema pia walifanya safari za kusafirisha mizigo kwenda nchi ya Comoro.

Alisema kupitia safari hizo, ATCL walipata mapato ambayo pamoja na mambo mengine yaliwawezesha kulipa mishahara ya wafanyakazi.

Alisema kwa sasa hali imeanza kuwa nzuri hasa kwa soko la ndani na wamefikia asilimia 90 ya miruko yake.

Kuhusu safari za nje, alisema wameanza katika vituo vya Lusaka nchini Zambia, Harare nchini Zimbabwe, Mumbai huklo India, Comoro na Entebbe nchini Uganda. Alisema muda si mrefu watarudi Bujumbura nchini Burundi.

Kuhusu safari ya Guangzhou nchini China, ilikuwa waanze mwezi Machi mwaka huu, lakini ilisogezwa mbele hadi mwezi Septemba kutokana na Covid-19. Lakini nayo haikuwezekana kutokana na masharti ambayo hayakuwa rafiki kwao kibiashara, hivyo waliamua waendelee kusubiri; na hali itakapokuwa nzuri, safari hiyo itaanza.

Chanzo: habarileo.co.tz