Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ATCL yapima mizigo kisasa kuongeza mapato

Ae537bea0a7cf4aa82ed336b254ac499 ATCL yapima mizigo kisasa kuongeza mapato

Mon, 25 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

KAMPUNI ya Ndege Tanzania (ATCL) imeshafunga na kuanza kutumia mfumo wa kisasa wa kupima mizigo kama inavyofanyika kwenye mashirika mengine makubwa ya ndege .

Taarifa ambazo HabariLEO inazo ni kwamba mashirika mengine makubwa ya ndege yanayofanya safari zake hapa nchini yana mfumo wa kisasa wa kupima mizigo ya abiria ambapo kilo zinazozidi zinapigiwa hesabu kielektroniki na kutoa gharama ya jumla ambayo mteja huilipa papo hapo.

Imeelezwa kuwa kupitia mfumo huo, endapo mteja atakuwa hajakamilisha malipo yake, anapofika kwenye ndege, pasi yake ya kupandia kwenye ndege (Boarding pass) inapopigwa panchi inagoma.

Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi, aliliambia HabariLEO kuwa ATCL imeshafunga na kuanza kuutumia mfumo huo tangu Novemba mwaka jana.

Matindi alikiri kuwa awali mteja alikuwa akiandikiwa risiti za kawaida kwa kilo zilizozidi lakini kwa sasa utaratibu huo haupo baada ya kufunga mfumo wa kisasa wa kupimia mizigo kama ilivyo kwa mashirika mengine makubwa ya ndege.

“Zamani ilikuwa unampimia mtu lakini ilikuwa haioneshi kwenye mfumo uzito uliozidi, lakini sasa hivi ukipimiwa mzigo wako inaonesha kama ni kilo 20 na kilo 10 zimezidi na unatakiwa ulipie,” alisema Matindi.

Matindi alisema mfumo wa zamani ulikuwa hatarishi kwa sababu endapo kama kungekuwa na mtu siyo mwaminifu na mjanja mjanja angeweza kuiba kidogo lakini kwa sasa usimamizi ni mzuri na kihatarishi hicho hakipo.

Japo hakuwa na takwimu kwa wakati huo, Matindi alisema mfumo mpya umeongeza kwa kiasi kikubwa mapato ikilinganishwa na zamani.

Chanzo: habarileo.co.tz