Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ATCL yapasua anga kupeleka mizigo China

Dc7f300aa12caf40da5f1f7832dc060e.jpeg Air Tanzania

Tue, 10 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

UBALOZI wa Tanzania nchini China umehimiza Watanzania kutumia ndege za Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) kusafirisha mizigo moja kwa moja kutoka Dar es Salaam hadi Guangzhou nchini China.

Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki, alisema hayo katika mkutano na Watanzania wanaoishi na kufanya biashara nchini China.

Alisema ATCL imeanza safari za kusafirisha mizigo kutoka mji wa Guangzhou hadi Dar es Salaam na safari ya kwanza ilianza mwishoni mwa wiki iliyopita na kwamba, ndege ya ATCL iliingia jijini humo saa saba usiku.

Alisema kwa njia ya mtandao kuwa, ndege hiyo ilishusha mzigo salama na kupakia mzigo wa kurudi Tanzania.

“Tuoneshe uzalendo kwa kuunga mkono shirika letu la ATCL, chako ni chako, cha mwingine ni cha mwingine, tuaminini shirika letu, tulipeni kazi na kulitumia ili tusonge mbele,”alisema Kairuki.

Alisema ATCL walipewa kibali cha kusafirisha mizigo mara moja kwa wiki, lakini kwa kuwa watu wengi hawafahamu kuanza kwa safari hizo, ndege ya shirika hilo itafanya safari moja kwa wiki mbili.

“Nitoe rai kwa Watanzania wenzangu hususan ninyi mnaofanya shughuli za kusafirisha mizigo, tutumie ndege yetu ya ATCL kusafirisha mizigo kwa sababu tuna uhakika wa mizigo kwenda moja kwa moja.”

“Mzigo unatoka hapa China moja kwa moja kwenda Zanzibar au Dar es Salaam na kama unaenda kwenye vile vituo vingine, utaweza kuusafirisha mzigo wako kwa usalama,” Balozi Kairuki.

Alisema ATCL pia itakuwa ikifanya safari kama hizo katika nchi nyingine katika miji ya Entebbe nchini Uganda, Lusaka-Zambia, Harare-Zimbabwe na Comoro.

Kwa mujibu wa Balozi Kairuki, kila baada ya wiki mbili ndege ya ATCL itaondoka Dar es Salaam Ijumaa saa tano na dakika 10 asubuhi na kuwasili Guangzhou Jumamosi saa tisa na dakika 10 alfajiri.

Alisema ndege hiyo itaondoka Guangzhou Jumamosi hiyo hiyo saa 11 alfajiri na kufika Dar es Salaam Jumamosi saa tano na dakika 10.

Kwa mujibu wa Balozi Kairuki, ndege hiyo itasafirisha mizigo aina zote isipokuwa bidhaa za hatari zikiwemo betri na mbolea.

Alisema kutokana na Covid-19, gharama za kusafirisha mizigo kwa meli zimekuwa kubwa kwa kuwa kampuni za meli zimepunguza idadi ya meli zinazotoka China kuja Tanzania na kutoka China kwenda sehemu nyingine za dunia.

Balozi Kairuki alisema kabla ya Covid-19 kontena la futi 20 nchini lilikuwa likisafirishwa kwa Dola 1,500 hadi Dola 2,000, lakini sasa linasafirishwa kwa Dola 9,000 hadi Dola 10,000.

Alisema usafirishaji wa kontena kutoka Shangai China kwenda Los Angeles -Marekani ulikuwa Dola 300, lakini wiki iliyopita ilifikia Dola 30,000.

Chanzo: www.habarileo.co.tz