Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ATCL yakwama safari za nje

37947 Pic+ATCL ATCL yakwama safari za nje

Wed, 23 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limesema mpaka sasa limeshindwa kuanza safari zake nje ya nchi kwakuwa bado linakamilisha baadhi ya taratibu ikiwa ni pamoja na kuunganishwa na mitandao mikubwa ya uuzaji tiketi ulimwenguni.

Shirika hilo limekuwa likitangaza kuanza kwa safari zake mbalimbali za kimataifa ikiwamo kwenda Mumbai India na Guangzhou China, lakini mpaka sasa halijafanya hivyo licha ya kurudishiwa uanachama wa shirikisho la mashirika ya ndege duniani (IATA).

Akizungumza na Mwananchi jana, mkurugenzi mtendaji wa ATCL, Ladislaus Matindi alisema licha ya kuwa walirudishiwa uanachama, kuna madai mengine yalijitokeza kuhusu mambo ya kisheria lakini sasa yamekwisha kamilishwa.

“Tulirudishiwa uanachama tukajua ndio tumemaliza lakini yalikuja madai mengine ambayo yalihitaji uchunguzi, yamekwisha kamilika na sasa tunamalizia kuunganishwa na mifumo mikubwa ya uuzaji wa tiketi duniani, kati ya mifumo mitano tumeunganishwa na mitatu bado miwili,” alisema.

Matindi alisema wakati ndege za masafa marefu zikinunuliwa mchakato wa kuuanza kutumia jukwaa la IATA ulikuwa unaonekana unakamilika mapema lakini kuna mambo yalijitokeza ndani ya shirikisho hilo ikiwamo vibali vya nchi ndege inakotarajia kutua na kusababisha kutoanza kwa safari hizo mpaka sasa.

Hata hivyo, alisema taratibu zilizobaki zitakamilika mwezi Februari na kabla ya kuisha kwa mwezi huo tiketi za kwenda China na India zitakuwa zinauzwa na tarehe ya safari ya kwanza itakuwa imepangwa.

“Hivi sasa kuna safari tatu za kimataifa, Comoro inalipa sana kila ndege inaposafiri inakuwa imejaa kwa asilimia zaidi ya 70, soko linalofuata kwa ukubwa ni Burundi, Uganda bado soko sio zuri lakini ni mapema kulitathimini pengine kutouza tiketi zetu IATA ndiyo sababu baada ya hapo soko litaimarika,” alisema.

Aidha, Matindi alisema ndege mbili zilizokuwa zikitumiwa na Rais ambazo walipewa ili wazitumie kibiashara zitasaidia kufika katika maeneo yenye abiria wachache na kuwaunganisha na ndege kubwa zenye abiria wengi.



Chanzo: mwananchi.co.tz