Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ATCL yaingia makubaliano ya kibiashara na NMB

Zaipuna Pic ATCL yaingia makubaliano ya kibiashara na NMB

Wed, 16 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Shirika la ndege Tanzania ATCL limeingia makubaliano ya Kibiashara na benki ya NMB, ambapo kuanzia sasa wateja wote wa shirika hilo la ndege watakuwa na uwezo wa kukata tiketi zao kupitia matawi yote ya benki hiyo, pamoja na njia zake mbadala ikiwamo NMB mkononi na NMB wakala.

Akizungumza kwenye hafla ya kutambulisha makubaliano hayo kati ya benki ya NMB na Shirika la ndege Tanzania, afisa mtendaji mkuu wa benki ya NMB Ruth Zaipuna amesema kuanzia sasa wateja na wale wasio wateja wa benki ya NMB ambao wanahitaji kusafiri kwa kutumia ndege za shirika la ndege Tanzania, wanauwezo wa kukata tiketi zao kupitia matawi yote 229 ya benki hiyo yaliyosambaa kote nchini.

"Ni imani yetu sisi NMB kwamba, huduma hii sio tu inaenda kumpa urahisi na wepesi msafiri wa kulipia tiketi yake, bali kumkinga pia na majanga yatokanayo na safari kama ulemavu, kifo na upotevu wa mizigo" amesema Zaipuna.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Mhandisi Ladislaus Matindi, aliipongeza NMB sio tu kwa ushirikiano wao huo, bali kuweka ziada ya Bima ya Safari kwa wateja wao, huku akibainisha kwamba hakuna tena sababu ya Watanzania kusafiri kwa hofu wakati kuna ATCL na NMB.

"ATCL kila siku tumejikita katika kuboresha utoaji huduma zetu, kuanzia tiketi inapokatwa, mteja anapokuwa safarini hadi kufika, hivyo tunajivunia ushirikiano wetu na NMB, ambao unaenda kututofautisha na watoa huduma za usafiri wa anga wengine waliopo sokoni" amesema Matindi.

Matindi alienda mbali zaidi na kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kila aina ya uwezeshaji inaowapa katika kutoa huduma kwenye Sekta ya Usafiri wa Anga kitaifa na kimataifa, ambako kufikia mapema mwakani watatanua mtandao wa ndege zao kufikia 16.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live