Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) leo Mei 23, 2022, limezindua ratiba mpya ya safari ya ndege kwenda mkoani Katavi, kutoka safari tatu hadi nne.
Akizindua ratiba ya safari hiyo mpya, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko amesema kuongezeka kwa safari hiyo kumekuja muda muafaka baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuzindua filamu ya Royal Tour.
Amesema filamu hiyo itasaidia kuongeza watalii mkoani humo katika hifadhi ya Taifa ya Katavi na vivutio vingine vinavyopatikana mkoani humo kama Mto Mapacha, twiga mweupe, maporomoko na misitu ya asili, hivyo kuchochea uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.
Awali akitoa taarifa katika uzinduzi huo, Meneja wa ATCL Mpanda, Peter Kilawe amesema wamefanya hivyo kutokana na maombi ya wadau yaliyochangiwa na ongezeko la abiria.
Amesema Mkoa wa Katavi una muingiliano na nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi na Zambia, hivyo mzunguko wa wafanyabiashara unakuwa mkubwa.
Kwa sasa ratiba ya ndege kutoka Mpanda, Tabora- Dar es Salaam itakuwa Jumatatu, Jumanne, Alhamisi na Jumamosi.