Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ATCL kuwekwa kitimoto uahirishaji safari bila taarifa

63633 Atcllpic

Fri, 21 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baraza la Ushauri la Wasafiri wa Anga (TCAA CCC) limesema Mbali na Profesa Mark Mwandosya, kuna malalamiko tofauti kutoka kwa abiria wengi wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

Ofisa mtendaji mkuu wa TCAA CCC, Kikoyo Rugambwa amesema wamepokea malalamiko hayo na wanachukua hatua.

“Leo  tutakutana ATCL kuzungumzia suala hili. Abiria wengi wana malalamiko tofauti,” alisema Rugambwa.

Hatua hiyo inafuatia kuwapo Kwa malalamiko kutoka kwa abiria wanaotumia ndege za ATCL kuhusu mabadiliko ya ratiba za safari bila ya kutolewa taarifa.

Aliyekuwa mbunge wa Rungwe mpaka mwaka 2015 na waziri kwa nyakati tofauti, Profesa Mark Mwandosya aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter (@MarkMwandosya) juu ya ndege yake kucheleweshwa.

Katika ujumbe aliouandika Juni 18, 2019, profesa huyo amesema alipaswa kusafiri Mei 29 kutoka Dar es Salaam kwenda Entebbe, Uganda lakini licha ya kufika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) saa 1:00 asubuhi kwa safari iliyokuwa ianze saa 4:30 asubuhi, ilisogezwa mbele mpaka saa 9:00 alasiri.

Pia Soma

Hali ilikuwa tofauti pia wakati anarudi Mbeya akitokea Dar es Salaam kwani ilikuwa asafiri saa 4:20 asubuhi na alifika JNIA saa 1:15 lakini akaambiwa ndege ilishaondoka saa 1:00 asubuhi.

“Huu ni utaratibu mpya au ni kukosa ushindani?” amehoji Profesa Mwandosya.

Hata hivyo, akizungumza na gazeti hili, Profesa Mwandosya alipongeza juhudi za Serikali kulifufua shirika hilo tena kwa kununua ndege mpya. “Hili ni suala dogo ambalo linaweza kurekebishika. Tunalipenda shirika letu na tungefurahi kuona huduma zake zinakuwa za viwango vya juu,” alisema.

Kwa utaratibu hasa wa safari za kimataifa, abiria anapaswa kufika uwanja wa ndege saa tatu kabla ya muda wa kuondoka.

Akijibu tuhuma za abiria, Mkurugenzi mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi alisema mabadiliko ni kawaida kwenye usafiri wa anga na mtoa huduma hutakiwa kubeba dhamana ya usumbufu utakaojitokeza.

Alisema shirika linaweza kuahirisha safari au kusogeza muda mbele lakini lolote litakalofanywa linapaswa kujulishwa kwa abiria husika.

“Ukiwa amtandaoni huwezi kukata tiketi mpaka ujaze namba yako ya simu. Tunawaomba abiria wetu waandike namba zinazopatikana ili kukiwa na mabadiliko tuwajulishe kwa wakati lakini wengi huwa hatuwapati tukitaka kuwajulisha mabadiliko yaliyopo,” alisema Matindi.

Kwa mujibu wa TCAA CCC, abiria wa shirika hilo wanalalmikia kubadilishwa kwa muda wa safari bila kupewa taarifa kwa wakati na huduma zisizoridhisha kutoka kwa wahudumu.

“Mimi mwenyewe nimewahi kucheleweshwa. Kuna wakati nilikuwa nasafiri kutoka Kilimanjaro kuja Dar es Salaam. Ndege haikufika kwa wakati hivyo tukalazimika kuisubiri,” alisema Rugambwa.

Wadau hao wanasema hoja ya kutopatikana kwa abiria pindi wanapotafutwa haina mashiko kwani haiwezekani zaidi ya abiria 20 wasipate taarifa.

“Nilikuwa nasafiri na mke wangu kwa ndege ya asubuhi lakini tulikalishwa uwanja wa ndege mpaka jioni ndipo tukaondoka. Kuna watu walikuwa na watoto wadogo, ni usumbufu kwa kweli,” alisema abiria ambaye hakutaka kutajwa jina gazetini.

Hata hivyo, Matindi alisema wanapaswa kushughulikia kero zote zinazojitokeza ili kutowapoteza abiria wao. “Wanaweza kwenda Precision au wakaamua kutumia mabasi ya mikoani. Tunafahamu ushindani uliopo na tunachukua hatua. Wateja wetu ni watu muhimu sana,” alisema.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz