Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ATCL: Corona changamoto mpya kwenye biashara

98812 ATCL+PIC ATCL: Corona changamoto mpya kwenye biashara

Fri, 13 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Shirika la ndege la Tanzania (ATCL) limesema maambukizi ya virusi vya corona ni miongoni mwa changamoto mpya wanayokumbana nayo katika biashara.

Akizungumza leo Jumatano Machi 12, 2020 katika ufunguzi wa mkutano wa tano wa baraza la wafanyakazi wa ATCL mkurugenzi mtendaji  wa shirika hilo,  Ladislaus Matindi amesema mlipuko wa virusi hivyo umesababisha kuahirishwa kwa safari za kukodi na uzinduzi wa safari za China.

“Tunaendelea vizuri lakini tuna changamoto kadhaa moja wapo ni mlipuko wa virusi vya corona, vimevuruga safari yetu ya kukodiwa na wachina, pia Aprili 2020 tulikuwa tuanze safari za Guangzhou kupitia Bangkok lakini tutashindwa kufanya hivyo,” amesema Matindi

Amesema mbali na safari hizo mbili hakuna safari nyingine iliyoahirishwa na ni vigumu kujua ATCL itapata hasara kiasi gani kutokana na mlipuko huo lakini kwa safari za China ambazo zimeahirishwa zilikuwa zinatarajia kuchangia asilimia 2 hadi 3 ya mapato ya shirika.

Amebainisha kuwa changamoto nyingine zinazolikabili shirika hilo ni ukosefu wa taa katika baadhi ya viwanja vya ndege jambo linalosababisha washindwe kufanya biashara usiku na mchana pamoja na mzigo wa madeni ambayo ATCL inadaiwa huko nyuma.

Kwa upande wake naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta  Nditiye amesema ili kuzikabili changamoto zilizopo Serikali iko tayari kuwaunga mkono.

Pia Soma

Advertisement
Amesema Serikali bado haijapiga marufuku safari za ndege kutoka nchi yoyote inachokifanya ni kudhibiti abaria wanaoingia lakini inaendelea kufuatilia kwa karibu na endapo hali itakuwa ya kutisha zaidi haitasita kusitisha safari.

“Tunazingatia sana suala la usalama hatutaendelea kuruhusu safari za ndege zetu kwenye mataifa mengine au zinazokuja nchini endapo hali itakuwa mbaya, lakini hali ikiwa mbaya hata abiria watapungua sana na mizigo pia,” amesema.

Amesema mlipuko wa virusi hivyo unatarajia kuathiri sekta ya usafiri wa anga dunia nzima na kwa mujibu wa shirikisho la kimataifa la mashirika ya ndege (IATA) mapato katika sekta hiyo yatapungua kwa zaidi ya Dola bilioni 100.

Chanzo: mwananchi.co.tz