Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

AI kuathiri asilimia 60 ya ajira za nchi tajiri

Articial Intellegnce.png AI kuathiri asilimia 60 ya ajira za nchi tajiri

Mon, 15 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Nchi zilizoendelea zinatarajiwa kukumbwa na athari ya asilimia 60 katika ajira zake, kutokana na kuingia kwa teknolojia ya akili bandia (AI).

Hayo yameelezwa leo Jumatatu, Januari 15, 2024 na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), Kristalina Georgieva alipozungumza katika mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF).

“Mataifa yaliyoendelea kiuchumi na yenye masoko makubwa, yatakabiliwa na athari katika ajira zake kwa asilimia 60,” amesema akinukuu ripoti ya IMF iliyochapishwa jumapili.

Amesema kwa nchi zenye uchumi wa chini ajira zitakazoathiriwa na teknolojia hiyo ni asilimia 26 pekee na kwamba athari katika ulimwengu mzima itakuwa ni asilimia 40.

Ripoti ya IMF inaeleza karibu nusu ya ajira zitakumbwa na athari hasi, huku nyingine zikizaa matokeo chanya yanayotokana na ongezeko la ufanisi na uzalishaji kupitia teknolojia ya AI.

"Kazi zenu ama zinaweza kupotea au AI inaweza kuziboresha zikawa na tija zaidi na kipato kitaongezeka,” amesema mkurugenzi huyo.

Kulingana na IMF, mwanzoni teknolojia hiyo itaathiri masoko yanayoibukia na nchi zinazoendelea kiuchumi, kadhalika zitachelewa kufaidika kutokana na kutokuwa na teknolojia hizo.

"Hii inaweza kuzidisha mgawanyiko wa kidijitali na tofauti ya mapato ya nchi mbalimbali," ripoti hiyo inaeleza.

Hata hivyo, Georgieva amesema ni muhimu mataifa yakawa na sera zinazosaidia kuendana na teknolojia hizo ili kukabiliana na athari tarajiwa.

“Lazima tujikite katika kuzisaidia nchi za kipato cha chini hasa zisonge mbele kwa kasi ili kupata fursa zitakazotokana na akili bandia.

"Akili bandia ndiyo, inatisha kidogo. Lakini pia ni fursa kubwa kwa kila mtu," amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live