Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

AGRICOM yatahadharisha wakulima zana duni kilimo

AGRICOM AGRICOM yatahadharisha wakulima zana duni kilimo

Tue, 23 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

TAASISI ya AGRICOM Afrika LTD inayojihusisha na usambazaji wa zana mbalimbali za kilimo, imewataka wakulima nchini kuachana na matumizi ya zana duni za kilimo likiwamo jembe la mkono na badala yake watumie zana za kisasa ambazo zitawasaidia kulima maeneo makubwa na kuongeza tija.

Rai hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na mwakilishi wa taasisi hiyo, Cecilia Julius wakati wa Mkutano wa Asasi ya Uwezeshaji wa Sekta Binafsi ya Kilimo (Pass Trust) na wadau wa kilimo, mifugo na uvuvi.

Cecilia alisema kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanayoendelea duniani, Watanzania wanatakiwa kuendana nayo ili kuwa na uwezo wa kuzalisha mazao kwa wingi na kuongeza kipato.

Alisema taasisi hiyo ina mashine mbalimbali za kisasa ambazo zinafanya kazi kuanzia kwenye uandaaji wa mashamba mpaka kwenye uvunaji, hivyo zinarahisisha kazi na kumfanya mkulima kulima eneo kubwa kwa wakati mfupi.

“Hizi mashine tunaziuza kwa pesa taslimu ama kwa mkopo na tumeshajiunga na wenzetu Pass Trust, ili kuwarahisishia wananchi upatikanaji wa mikopo ya vifaa vyetu kwa sababu wenzetu hawa wanadhamini mikopo kwa wakulima,” alisema.

Cecilia alizitaja baadhi ya mashine ambazo taasisi hiyo inazo kuwa ni matrekta, 'combine' za kuvunia, majembe ya kuvutwa na ng’ombe pamoja na mashine za kupandia mahindi na mpunga.

Aliwashauri wakulima kuchangamkia mikopo ya vifaa hivyo kwa maelezo kuwa urejeshaji wa mikopo hiyo ni wa taratibu na baadhi inachukua miaka kadhaa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Pass Trust, Nicomed Bohay, alisema wanashirikiana na taasisi hiyo na Benki ya Maendeleo ya Kilimo kuwasaidia wakulima kupata mikopo.

Alisema ili mkulima asaidiwe na Pass kukopeshwa mashine ama pesa, ni lazima awe na uwezo wa kujidhamini kwa angalau asilimia 20 ya mkopo wote na kwamba asilimia nyingine inayobaki anadhaminiwa na Pass Trust.

“Wenzetu AGRICOM wanasambaza hizi zana za kilimo, lakini taasisi za fedha zinakopesha pesa, hivyo tukiziunganisha taasisi zote hizi, tuna uhakika wa wakulima wetu kuongeza uzalishaji,” alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, alizishauri taasisi zote zinazotoa mikopo kwa wakulima katika mkoa huo kuweka masharti nafuu, ili kuwawezesha wakulima wengi zaidi kukopa kwa ajili ya maendeleo ya kilimo na uchumi.

Aliishauri AGRICOM Afrika kuziuza mashine zake kwa bei nafuu, ili wakulima wengi zaidi wamudu kuzinunua na kuzitumia kwenye uzalishaji.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live