Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

AGRA,TAPBDS watoa ruzuku ujenzi kiwanda cha kuchakata mazao

WhatsApp Image 2021 06 21 At 12.45.13.jpeg AGRA,TAPBDS watoa ruzuku ujenzi kiwanda cha kuchakata mazao

Tue, 22 Jun 2021 Chanzo: ippmedia.com

Kupitia Mradi wa kusaidia kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno unaoendeshwa na TAPBDS, AGRA imetoa mitambo ya takribani Sh. milioni 100 kwa kiwanda cha kutengeneza mashine cha Nondo mkoani humo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mtambo huo, Meneja Mradi kutoka TAPBDS, Joshua Ongaga, amesema lengo la kutoa mitambo hiyo ni kuongeza uzalishaji wa mashine za kuchakata mazao na kurahisisha upatikanaji wake kwa wafanyabiashara na wakulima kwa bei nafuu.

Ongaga amesema awali wafanyabiashara walikuwa wakinunua mashine hizo kwa Sh. milioni 2 lakini kwa sasa mashine hizo zitanunuliwa kwa Sh. 900,000.

Amesema mashine zitakazotengenezwa kupitia mitambo hiyo ni za kusaga mahindi, kukoboa mpunga, kupukuchua maharage, kukamua mafuta ya alizeti pamoja na kuchonga vipuli mbalimbali ili kuongeza thamani ya mazao na kukuza uchumi wa wakulima.

Amefafanua kuwa mbali na mitambo hiyo ya Nondo, walitoa mingine minne katika mikoa ya Ruvuma, Njombe, Mbeya na Rukwa ambayo yote thamani yake ni zaidi ya Sh. milioni 600.

Mbali na ruzuku ya mitambo kwa wazalishaji wa mashine, mradi huo umewezesha pia wafanyibiashara 31 kutoka mikoa ya Kagera, Kigoma, Ruvuma, Njombe, Iringa, Rukwa na Katavi kwa kuwapa mashine za kuchakata mazao. 

“TAPBDS tunaamini kuwapo kwa mradi huu kutasaidia sekta ya kilimo nchini, kuongeza thamani ya mazao na wakulima kunufaika na kilimo moja kwa moja,” amesema Ongaga kwa niaba ya mkurugezi wa TAPBDS.

Kwa upande wake, Mkurugenzi na Mmiliki wa Nondo Investment, Raymond Kamtoni, amesema kampuni inakusanya mazao kutoka kwa mtandao wa wakulima, vyama vya ushirika na wakulima wenyewe.

Amesema wameajiri wataalam wa kilimo sita kwa ajili ya kutoa elimu kwa wakulima ya kulima kilimo chenye tija na kitakiacholeta manufaa kwao.

Kuhusu kiwanda, amesema kina uwezo wa kusaga mahindi tani 25, mpunga tani 20 na mafuta ya alizeti tani tano hadi 10 kwa mwezi na wana mpango wa kufunga mashine nyingine ya kuchuja hadi tani 20.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Katavi, Mwamvua Mrindoko, akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi huo, amesema mkoa wake unategemea kilimo kwa asilimia 90 hivyo kupitia mradi huo unaenda kukuza uchumi wake kwa kasi.

Amesema wakulima wataongeza kipato kwa sababu watapata mazao mengi kutokana na kutumia mfumo mpya wa kupukuchua, kukoboa na kusaga kwa mashine za kisasa.

Amesema awali walikuwa wanatumia mfumo wa zamani wa kupiga mazao wakati wa kuyapukuchua hivyo kusababisha mengi kupotea. 

Chanzo: ippmedia.com