Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ACT yataja mambo 7 kuimarisha kilimo nchini

Marekani Inashirikiana Na Kenya Katika Sekta Ya Kilimo ACT yataja mambo 7 kuimarisha kilimo nchini

Wed, 9 Aug 2023 Chanzo: mwanachidigital

Chama Cha ACT Wazalendo kimetaja mambo saba yanayopaswa kuboreshwa ili kuimarisha sekta ya kilimo kwa manufaa ya wakulima na Taifa. Mambo hayo ni pamoja na kulinda uhuru wa wakulima juu ya uzalishaji na soko la mazo ya kilimo, kuimarishwa uhakika wa upatikanaji, umiliki na matumizi ya ardhi ya kijiji na kuanzishwa kwa viwanda vidogo vijijini.

Mengine ni kutungwa kwa Sheria ya kilimo ili kuwe na mifumo ya kikodi ya kisheria, kufungamanisha kilimo na viwanda, kuchochea uzalishaji wa mbolea nchini na kuimarisha ushirika.

Hayo yameelezwa leo Agosti 8 na Msemaji wa Sekta ya Kilimo, Umwagiliaji na Maendeleo ya Ushirika wa ACT, Mtutura Mtutura kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa leo akisema ili kuwe na mafanikio katika sekta hiyo, lazima changamoto zilizopo zitatuliwe.

“Kilimo chetu kimetawaliwa na utumiaji wa nyenzo duni, kuzalisha bidhaa za kilimo kwa ajili ya soko la nje, kiwango cha utegemezi kwenye soko la nje ni kikubwa zaidi, kukosekana kwa uhakika wa bei za mazao pamoja na kutokuwepo kwa ruzuku za uzalishaji,” amesema.

Kutokana na hali hiyo ameshauri kuboresha mfumo wa uzalishaji.

“Ni ukweli kwamba bado Tanzania ni nchi ya wakulima, wafugaji na wazalishaji wengine wadogo waishio vijijini na mijini wanaotegemea mnyororo wa thamani wa kilimo.

“Maendeleo ya nchi ni kuinua hali ya maisha ya asilimia 65 ya Watanzania wenzetu kwa kuboresha mfumo wa uzalishaji na kubadili uhusiano wa sasa,” amesema.

Kuhusu mchango wa wakulima kwa chakula, malighafi za viwanda na kuingiza fedha za kigeni, amesema ni wakulima wadogo kwa asilimia 100 ndio huchangia.

Aidha, zaidi ya asilimia 61 wameajiriwa katika sekta ya kilimo lakini bado kuna changamoto kama uporaji wa ardhi ya vijiji na wakulima kwa kigezo cha uwekezaji katika Kilimo, tishio la kuporwa kwa uhuru wa wakulima katika uzalishaji, uhifadhi wa mbegu na mazao ya kilimo kupitia dhana ya kilimo biashara.

Vilevile, imeeleza uwepo wa tija ndogo katika uzalishaji kunakosababishwa na matumizi hafifu ya teknolojia ya wakulima wenyewe.

Kwa kushauri ACT imesema lazima hatua za makusudi zichukuliwe kwa ajili ya kufanya mapinduzi katika kilimo kwa kuifungamanisha sekta ya kilimo na viwanda.

Kutokana na hali hiyo ameshauri wakulima wapewe uhakika wa kumiliki ardhi kwa lengo lakuzalisha au kukidhi haja ya kijamii na sio kulimbikiza faida, kuwekea rehani (dhamana).

“Serikali isimamie kuanzishwa kwa viwanda vidogo maeneo ya vijijini vinavyoendeshwa, kumilikiwa na kusimamiwa na wakulima wenyewe kupitia vyama vyao vyao vya ushirika ambavyo vitaweza kuzalisha ajira na kuchakata mazao,” amesema

Chanzo: mwanachidigital