Asilimia 86 ya maziwa yanayozalishwa nchini hayako katika soko rasmi hivyo kusababisha walaji kutokuwa na imani na bidhaa hiyo. Kauli hiyo imetolewa na Msajili wa Bodi ya Maziwa, Dk George Msalya wakati wa kufungua kikao kazi chenye lengo la kubainisha vipaumbele ambavyo vitawekezwa ili kuleta matokeo chanya sekta ya maziwa.
Majadiliano hayo ni sehemu ya kutekeleza mradi wa kujenga uwezo kwa ajili ya utekelezaji na ufuatiliaji wa Mpango Kabambe wa Sekta ya Mifugo.
“Maziwa yasiyo katika mfumo rasmi ubora wake unakuwa haujulikani hivyo kufanya walaji kutokuwa na imani na bidhaa hiyo, hivyo nitoe wito watu kufuata takwa la sheria kwa kuingiza maziwa mengi kwenye soko rasmi,” alisema na kuongeza: “Kwa sasa kuna vituo 220 vya kukusanya maziwa lakini bado maziwa hayakusanywi na hayafiki kwenye vituo, najua kuna changamoto kadhaa, sasa kikao hiki kiangalie namna ya kuja na suluhisho ili maziwa mengi yaingie kwenye mfumo rasmi tuwe na maziwa bora ambayo yanawafikia walaji na wayatumie bila kukiwa na mashaka yoyote,” alisema.
Alisema sekta ya mifugo imeendelea kukua na kuifanya Tanzania kushika nafasi ya pili barani Afrika kwa kuwa na mifugo mingi ambapo ina ng’ombe milioni 33.9 huku zaidi ya kaya milioni 2 zinajihusisha na shughuli za ufugaji. “Tunahitaji uwekezaji wenye tija, lakini tunataka idadi kubwa ya mifugo tuliyonayo ichangie zaidi katika uchumi wa nchi katika Pato la Taifa na uchumi wa mtu mmoja mmoja au kaya moja moja.”
Alisema katika kikao cha Oktoba kilibainisha maeneo 10 ya uwekezaji na kusisitiza kuwa ili kuwa na mafanikio ya haraka ni vyema kuwa na vipaumbele vichache kama vitatu ili kupata mchango wa haraka. Aidha, Dk Mlasya alisema sekta ya maziwa inaendelea kukua kwa asilimia 2, huku ikichangia Pato la Taifa kwa asilimia 2 na inachangia sekta ya mifugo kwa asilimia 30
“Bado tuko chini pamoja na kuwa na idadi kubwa ya mifugo hivyo kunahitaji uwekezaji mkubwa.” Aidha, Dk Msalya alisema tasnia ya maziwa inakabiliwa na changamoto ya kuwa na asilimia 86 ya maziwa wanayozalishwa kuwa katika soko lisilo rasmi wakati uchakataji wa maziwa ni asilimia tatu ya maziwa yanachakatwa kati ya lita bilioni 3.3 zinazozalishwa hivyo kuhitaji nguvu na uwekezaji katika eneo hilo.
Dk Msalya alisema pia kuna haja ya kuweka nguvu katika uwekezaji ili kuimarisha viwanda vya maziwa nchini ambavyo viko 104 na vikihitaji malighafi ya kutosha.